Sala ya Maandalizi:
Bwana wangu mpendwa na wa kimungu, ninapoanza kuchunguza dhamiri yangu, unisaidie kuiona roho yangu kama Wewe unavyoiona. Katika huruma Yako kamilifu, unanipenda jinsi nilivyo, ingawa dhambi yangu inanizuia kuyakabidhi maisha yangu Kwako kwa ukamilifu zaidi.
Nijalie kuiona dhambi yangu ili uweze kuniweka huru kwa upole kutoka katika vizuizi hivi vya upendo Wako. Nipe ujasiri na tumaini Kwako, Wewe uliye Upendo na Huruma yenyewe. Yesu, nakutumainia. Nihurumie. Amina.
Majivuno: Majivuno ni kuwa na maoni yasiyo ya kweli kuhusu sisi wenyewe, dhana isiyo ya kweli kuhusu kile ambacho sisi si.
Je, nina mtazamo wa kujiona bora kuliko wengine katika kufikiri, kusema au kutenda? Je, ninawadharau wengine kwa kujiona wa hadhi ya juu? Je, mwenendo wangu au namna ninavyojionyesha ina kiburi na inawaudhi wengine? Je, ninajiona kuwa juu ya wengine? Je, ninadai kutambuliwa? Je, ninatamani kuwa wa kwanza daima? Je, ninatafuta ushauri? Je, niko tayari kuukubali ushauri? Je, kwa namna yoyote mimi ni mtu wa kuwanyanyasa wengine? Je, nina mwelekeo wa kupenda kuwamwamrisha wengine? Je, ninawasema wengine vibaya? Je, nimewasemea wengine uongo? Je, ninatangaza makosa ya wengine? Je, ninatafuta kuwatupia wengine lawama huku nikijitetea mwenyewe? Je, kuna mtu ninayekataa kuzungumza naye? Je, kuna mtu ambaye sijazungumza naye kwa muda mrefu? Je, nina mazoea ya kubishana? Je, ninawaudhi wengine katika mabishano yangu? Je, katika mabishano ninajiona bora kuliko wengine kana kwamba ninajua kila kitu? Je, ninajishughulisha sana na jinsi wengine wanavyoniona? Je, ninachukulia mambo moyoni kwa urahisi? Je, ninaumia moyoni kwa urahisi?
Husuda: Husuda ni huzuni tunayoihisi kwa sababu ya mema yanayompata jirani yetu.
Je, ninahuzunika wengine wanapofanikiwa? Wanapofanikiwa katika michezo? Katika riadha? Je, ninafurahia kushindwa kwao? Je, ninahusudu utajiri wa wengine?
Uvivu: Uvivu ni aina ya woga na kuchukizwa, ambayo hutufanya tuzembee na kuacha kutimiza wajibu wetu badala ya kujitia nidhamu.
Je, ninapenda kupumzika kupita kiasi, huku nikipuuza wajibu wangu? Je, ninatenda kwa uvivu? Je, ninapenda sana kupumzika? Je, ninakaa au kusimama kizembe ninapoitikia sala? Je, ninapiga magoti kwa namna ya kujibweteka? Je, ninafurahia mazungumzo yasiyo na maana? Je, ninakosa bidii katika kumtumikia Mungu?
Tamaa mbaya za mwili: Tamaa mbaya za mwili ni kupenda raha zinazopingana na usafi wa moyo na mwili.
Je, nimetamani au kufanya mambo machafu? Je, nimefurahia kuendeleza mawazo au tamaa chafu? Je, nimesoma maandishi machafu, nimesikiliza muziki wenye maneno machafu, au nimetazama picha chafu, iwe katika picha zilizopigwa, kwenye televisheni, katika filamu au kwenye Intaneti? Je, nimechochea tamaa ya ngono ndani yangu au kwa mtu mwingine kwa kubusiana, kukumbatiana au kugusana kwa namna chafu? Je, nimefanya matendo machafu nikiwa peke yangu, yaani kujichua? Je, ninavaa mavazi yasiyo ya staha au ninajishughulisha kupita kiasi na mwonekano wangu? Je, ninatumia lugha chafu au ninasimulia au kusikiliza mizaha au hadithi chafu? Je, nimekubali tamaa za uzinzi hata katika mawazo yangu?
Tamaa ya mali: Tamaa ya mali ni kupenda mali za dunia hii kwa namna isiyo na kiasi.
Je, ninatumia fedha zangu kwa namna isiyofaa au kwa ubinafsi? Je, ninatimiza wajibu wangu wa haki kwa binadamu wenzangu? Je, ninatimiza wajibu wangu wa haki kwa Kanisa?
Ulafi: Ulafi ni kupenda kula na kunywa kwa namna isiyo na kiasi.
Je, ninakula ili niishi au ninaishi ili nile? Je, ninakunywa pombe kupita kiasi? Je, ninalewa? Je, ninatumia vibaya dawa nilizoandikiwa na daktari? Je, ninatumia dawa za kulevya zilizopigwa marufuku? Je, nimejiruhusu kuwa mraibu wa pombe na/au dawa za kulevya?
Hasira: Hasira ni hisia ya rohoni inayotufanya tukatae kwa nguvu chochote kinachotuumiza au kutuchukiza.
Je, ninakasirika kwa urahisi? Je, karibu kila jambo dogo hunipandisha hasira? Je, ninashindwa kuzuia dalili za kwanza za hasira? Je, ninashindwa kuishi kwa amani na kila mtu? Je, ninayawaza sana matendo ya kudharauliwa au kuumizwa, na hata kudhani yametokea? Je, ninafurahia matatizo yanayowapata wengine? Je, ninafikiria njia za kulipiza kisasi? Za “kurudisha walichonitendea”? Je, nina tabia ya kupenda mabishano? Je, nina roho ya kupinga? Je, nina mazoea ya kuwadhihaki watu au kudhihaki mahali au vitu? Je, ni vigumu kuishi nami kwa amani? Je, ninaweka kinyongo na kuendelea kuwa katika uhasama na mtu yeyote? Je, ninazungumza kuhusu makosa ya wengine? Je, ninafichua makosa au kasoro za wengine? Je, ninafichua makosa ya wengine kwa nia mbaya?
Uchunguzi wa Dhamiri: Dhambi Kuu Saba
Uchunguzi wa Dhamiri: Amri Kumi
Uchunguzi wa Dhamiri wa Kila Wiki kwa Saa Takatifu
Uchunguzi wa Dhamiri: Imani, Matumaini & Mapendo
Uchunguzi Mfupi wa Dhamiri: Imani, Matumaini & Mapendo
Uchunguzi wa Jumla wa Dhamiri Kila Usiku
Kuchunguza Vilindi – Orodha Kamili ya Yaliyomo
Sehemu ya Kwanza: Historia ya Mtakatifu Inyasi na Mafundisho Kutoka Mazoezi ya Kiroho
Sehemu ya Pili: Tafakari za Kiinyasi Zilizopangwa Kulingana na Mwaka wa Liturujia
Sehemu ya Tatu: Nyenzo za Ziada za Sala za Kutumia Mwaka Mzima
