Kiswahili

Kusafisha Hekalu

Mpangilio wa Saa Takatifu

Somo la Maandiko Matakatifu: Yohane 2:13–25

Muktadha: Baada ya kusoma Maandiko Matakatifu hapo juu angalau mara moja, soma hoja zifuatazo zinazotoa mafundisho mafupi lakini yenye maelezo ya kina kuhusu Kutakaswa kwa Hekalu:

  • Sikukuu ya Pasaka ilikuwa sikukuu muhimu zaidi kila mwaka. Wanaume wote walitakiwa kufika mbele za Bwana. Wengi walifanya hivyo kwa kwenda hija Hekaluni ili kumtolea Mungu sadaka.
  • Waliokuwa matajiri walitoa kondoo au ng’ombe. Waliokuwa maskini walitoa hua au njiwa.
  • Kwa sababu ya Sikukuu hiyo, Hekalu lilijaa watu kupita kiasi, wengi wao wakijaribu kujipatia pesa kutokana na wajibu wa kidini wa kufika mbele za Bwana na kutoa sadaka.
  • Mtakatifu Ignasio anaeleza kwamba Yesu aliwafukuza wenye kubadilisha fedha na wale waliouza wanyama wakubwa kutoka Hekaluni kwa nguvu nyingi, lakini wale waliouza hua na njiwa walipewa tu himizo la kuwatoa Hekaluni.
  • Yesu anajitambulisha na Hekalu, akilita “nyumba ya Baba Yake.”
  • Wayahudi wanapoomba ishara inayoonyesha kwamba Yesu ana mamlaka ya kuwafukuza wote, anasema kwamba wakilibomoa Hekalu, Yeye atalijenga tena kwa siku tatu. Huu ni unabii kuhusu Yesu kufufuka kutoka kwa wafu siku tatu baada ya wao kumuua.
  • Yesu pia anaweka wazi kwamba “Hekalu” la kweli ni mwili Wake mwenyewe. Yeye ndiye Hekalu jipya ambamo ukamilifu wa Mungu unakaa.
  • Hekalu pia linaweza kueleweka kuwa ni nafsi zetu kwa kadiri Mungu anavyokaa ndani yetu. Tunakuwa hekalu la Mungu. Mojawapo ya kazi za utume wa Yesu ni kuondoa kwa ari kila dhambi katika nafsi zetu.

Tafakari: Soma tena simulizi hilo la Maandiko, kisha anza tafakari yako ya kina kwa kuyatafakari yafuatayo:

  • Tafakari kukaribia kwa Sikukuu hiyo. Wazia miezi na majuma yanayoitangulia. Wazia mipango na matarajio. Wafikirie wote waliohusika katika miezi iliyotangulia tukio hili: wenye kubadilisha fedha, wauzaji, matajiri, maskini, mahujaji wote, na Yesu pamoja na wanafunzi Wake.
  • Wazia hekaheka katika eneo la Hekalu lililofurika watu, harufu ya wanyama, kelele, tamaa ya mali, damu ya wanyama Hekaluni, joto kavu, na kadhalika.
  • Wazia Yesu akiwasili Hekaluni. Tafakari hasira ya haki inayomjaa anaposhuhudia nyumba ya Baba Yake ikinajisiwa.
  • Tafakari mjeledi wa kamba, Yesu akiwafukuza wanyama, akipindua meza, na kadhalika.
  • Sasa elekeza fikira zako kwenye hekalu la nafsi yako. Hilo pia ni nyumba ya Baba. Wewe ni makao matakatifu ya Mungu.
  • Ona pia dhambi na uchafu ambao umeruhusu kuingia katika nafsi yako. Unapofanya hivyo, mwone Yesu anapoiona dhambi hii na kutafuta kuiondoa kwa ari kubwa. Unaitikiaje? Je, kwa shukrani? Au unapinga?

Picha Iliyoangaziwa:Kristo Akitakasa Hekalu, na El Greco

Utangulizi wa Tafakari za Kipindi cha Mwaka

  1. Ubatizo wa Bwana
  2. Bendera Mbili
  3. Makundi Matatu ya Watu
  4. Majaribu
  5. Kuitwa kwa Mitume
  6. Arusi ya Kana
  7. Kusafisha Hekalu
  8. Hotuba ya Mlimani
  9. Kuituliza Dhoruba
  10. Kutembea Juu ya Maji
  11. Mitume Walitumwa Kuhubiri
  12. Kuongoka kwa Maria Magdalena
  13. Jinsi Kristo Alivyowalisha Watu Elfu Tano
  14. Kugeuka Sura kwa Kristo
  15. Kufufuka kwa Lazaro
  16. Karamu ya Jioni huko Bethania
  17. Njia Tatu za Unyenyekevu

Yaliyomo

Shiriki ukurasa huu: