
Divai ilipopungua, mama yake Yesu akamwambia, “Hawana divai.” [Naye] Yesu akamwambia, “Mwanamke, jambo linalokuhangaisha linanihusuje Mimi? Saa yangu bado haijafika.” Mama yake akawaambia wahudumu, “Fanyeni lolote atakalowaambia.” Yohane 2:3-5
Maneno haya yalisemwa na Mama yetu Mbarikiwa wakati wa muujiza wa kwanza wa Yesu: “Fanyeni lolote atakalowaambia.” Ni maneno yenye maana ya kina na nguvu, ambayo kwa urahisi yanaweza kuwa msingi wa maisha yetu ya kiroho.
Kama Mama yetu Mbarikiwa angesema jambo lolote kwa Mwanawe akiwa chini ya Msalaba, angesema nini? Je, angesema maneno ya kukata tamaa au kuchanganyikiwa, ya uchungu au hasira? La, angesema maneno yaleyale aliyosema kwenye Arusi ya Kana. Lakini wakati huu, badala ya kuwaambia watumishi maneno haya, angemwambia Mwanawe. “Mwanangu mpendwa, ninayekupenda kwa moyo wangu wote, fanya lolote ambalo Baba wa Mbinguni anakuambia.”
Bila shaka Yesu hakuhitaji ushauri huu, lakini hata hivyo alitamani kuupokea kutoka kwa mama yake. Alitamani kumsikia mama yake akimwambia maneno haya ya upendo mkamilifu. Kwa kuyatafakari maneno haya yaliyowahi kusemwa huko Kana, Mama yetu Mbarikiwa na Mwanawe wa kimungu wangekuwa wameshiriki umoja wa kina walipotazamana wakati wa uchungu Wake Msalabani. Mama na Mwana wote wawili walijua kwamba kifo Chake kilikuwa utimilifu wa wema mkuu kuliko wote uliowahi kujulikana. Wote wawili wangekuwa wamejua kwamba mapenzi ya Baba wa Mbinguni yalikuwa makamilifu. Wote wawili wangekuwa wametamani na kuyakubali mapenzi haya matakatifu bila kujibakiza. Na maneno haya yangekuwa mioyoni mwao wote wawili walipotazamana kimya:
“Mwanangu mpendwa, fanya lolote ambalo Baba Yako wa Mbinguni anataka ufanye.”
Tafakari leo maneno haya, na ujue kwamba mama na Mwana wanakuambia wewe pia. Haidhuru unakabili nini maishani, Mama yetu Mbarikiwa na Mwanawe wa kimungu wanakualika kuikubali amri hii tukufu ya upendo na utii. Wanakuhimiza ubaki mwaminifu katika mapambano yote, nyakati nzuri na nyakati ngumu, katika uchungu na furaha. Haidhuru unapitia nini maishani, maneno haya lazima daima yasikike akilini na moyoni mwako. “Fanya lolote atakalokuambia.” Usisite kuyasikiliza na kuyakubali maneno haya matakatifu.
Mama mpendwa sana, unatupa maneno ya hekima kamilifu. Unawaalika watoto wako wote wapendwa kuyakubali mapenzi makamilifu ya Baba wa Mbinguni. Maneno haya hayaambiwi mimi peke yangu. Kwanza uliambiwa wewe katika kina cha moyo wako. Nawe ukawapa wote uliokutana nao amri hii ya upendo. Pia, kwa ukimya ulimwambia maneno haya Mwanao mwenyewe wa kimungu.
Mama yangu mwenye upendo, nisaidie kukusikiliza unaponiambia maneno haya. Nisaidie, kwa nguvu ya sala zako, kuitikia mwito huu wa kuyakubali mapenzi makamilifu ya Mungu katika maisha yangu.
Yesu wangu wa thamani kuu, ninachagua kufanya yote unayoniagiza. Ninachagua mapenzi Yako bila kujibakiza, nami najua kwamba unanialika kufuata nyayo Zako. Nisikatishwe tamaa kamwe na magumu ya Msalaba, bali nibadilishwe kwa nguvu ya mapenzi Yako makamilifu.
Mama Maria, uniombee. Yesu, nakutumainia.
Siku ya Kumi na Tano – Kulisikia na Kulishika Neno la Mungu
Inapatikana kama Kitabu cha Kielektroniki & Kitabu chenye Jalada Laini!

