Kiswahili

Swali. Tafsiri mpya ya Misa Takatifu

Swali. Nakumbuka miaka michache iliyopita, katika mafundisho ya dini, tulizungumza kuhusu mabadiliko yaliyokuwa yanakuja katika Misa Takatifu. Mwalimu alisema kwamba maaskofu waliyafanyia kazi kwa miaka mingi kabla hayajaidhinishwa. Lakini mara tu baada ya Papa Fransisko kuchaguliwa, alimwongeza Mtakatifu Yosefu katika sala moja katikati ya Misa Takatifu. Kwa nini baadhi ya mabadiliko yalichukua miaka mingi na hili la karibuni zaidi likachukua takriban wiki moja?

Jibu. Aha, una uwezo mzuri sana wa kutambua mambo! Kwanza, nieleze kuhusu mabadiliko yaliyohusiana na tafsiri mpya, iliyoanza kutumiwa mwaka 2011, kisha nieleze kuhusu nyongeza iliyofanywa na Papa Fransisko.

Liturujia ilipotafsiriwa kutoka Kilatini kwenda Kiingereza na lugha nyingine, ilikuwa mara ya kwanza katika historia ya Kanisa (katika riti ya Kilatini) kwa Misa Takatifu kuadhimishwa kwa lugha nyingine isiyokuwa Kilatini. Tafsiri hiyo ilipofanywa mwanzoni mwa miaka ya 1970, kikundi kilichokabidhiwa kazi hiyo, yaani Tume ya Kimataifa ya Kiingereza katika Liturujia (au I.C.E.L), kililazimika kufanya kazi yake bila miongozo yoyote iliyo wazi. Bila shaka wote walioshiriki katika tafsiri walifanya kadiri ya uwezo wao, lakini bado, lilikuwa jaribio la kwanza na lilifanywa kwa haraka sana.

Kadiri miaka ilivyopita, watu wengi walianza kutoa mapendekezo na mawazo mapya kuhusu njia bora zaidi ya kutafsiri Liturujia kutoka Kilatini. Mwaka 1997, Papa Yohane Paulo II alitoa hati ambamo aliweka miongozo mipya kuhusu namna ya kutafsiri Liturujia. Kwa ujumla, aliomba tafsiri ziwe sahihi zaidi, badala ya kueleza kwa maneno mengine yaliyomo katika matini ya Kilatini. Hilo lilianzisha mchakato mrefu wa kutathmini, kujifunza, kujadiliana, kushauriana na kutafsiri upya. Wakati huu, Kanisa lilitaka kutoa tafsiri ambayo kila mtu angeikubali. Kila askofu katika maeneo ambako Kiingereza huzungumzwa alishauriwa, pamoja na wanazuoni wengi. Walitaka tu kufanya kazi hiyo ipasavyo. Kwa maoni yangu, matokeo ya mchakato huu mrefu sana ni tafsiri ya Kiingereza ya Misa Takatifu iliyo nzuri sana na yenye lugha ya hadhi ya juu. Kazi hiyo yote ngumu ya miaka mingi ilizaa matunda!

Kuhusu kuongezwa kwa jina la Mtakatifu Yosefu katika Sala zote za Ekaristi, hili ni jambo tofauti kabisa. Hili halikuwa suala la kuamua njia bora ya kutafsiri Liturujia nzima; bali lilikuwa suala la kuonyesha heshima na upendo wetu kwa Mtakatifu Yosefu katika Sala zote za Ekaristi, badala ya moja tu. Mwaka 1870, Papa Pius IX alimtangaza Mtakatifu Yosefu kuwa Mlinzi wa Kanisa lote. Amri ya Vatikani inasema kwamba Mtakatifu Yosefu “ni kielelezo bora cha wema na unyenyekevu ambavyo imani ya Kikristo huviinua kufikia hatima kuu, naye huonyesha fadhila za kawaida na rahisi zinazohitajika ili watu wawe wafuasi wema na wa kweli wa Kristo.” Mwaka 1962, Papa Yohane XXIII aliagiza jina la Mtakatifu Yosefu liingizwe katika Kanuni ya Kirumi, ambayo ndiyo Sala ya Kwanza ya Ekaristi na ilikuwa ndiyo pekee iliyokuwa ikitumika wakati huo. Kwa sababu fulani, Sala tatu za ziada za Ekaristi zilipoanza kutumika mwaka 1970, hazikuwa na jina la Mtakatifu Yosefu kama ilivyokuwa Kanuni ya Kirumi.

Inaonekana kwamba Papa Benedikto XVI alikuwa amepokea maombi mengi kutoka sehemu zote za Kanisa ya kuingiza jina la Mtakatifu Yosefu katika sala zote, kama Papa Yohane XXIII alivyofanya mwaka 1962 alipoingiza jina la Mtakatifu Yosefu katika Sala pekee ya Ekaristi iliyokuwa ikitumika wakati huo. Hatimaye Papa Benedikto XVI alikubali jambo hili, wakati uleule alipokuwa akijiuzulu wadhifa wa papa.  Papa Fransisko alichukua hatua haraka kutekeleza nia ya Papa Benedikto na akalitangaza jambo hili kwa amri rasmi. Kwa namna fulani, unaweza kusema kwamba mchakato huu ulianza mwaka 1962! Kwa hiyo ulikuwa mchakato mrefu zaidi kuliko ule wa kutafsiri upya Liturujia, ulioanza mwaka 1997 na kutekelezwa miaka kumi na minne baadaye.


Maswali na Majibu Zaidi kuhusu Imani Katoliki

Shiriki ukurasa huu: