
Leo najifungamanisha na
Jina lenye nguvu la Utatu,
Kwa kulitia Jina hilo,
Watatu katika Mmoja na Mmoja katika Watatu.
Leo najifungamanisha milele,
Kwa nguvu ya imani, na umwilisho wa Kristo;
Ubatizo Wake katika mto Yordani;
Kifo Chake Msalabani kwa wokovu wangu;
Kutoka Kwake kwa nguvu kaburini lenye manukato;
Kupaa Kwake katika njia ya mbinguni;
Kuja Kwake siku ya hukumu;*
Leo najifungamanisha na hayo.
Najifungamanisha na nguvu
Za upendo mkuu wa makerubi;
Sifa tamu ya ‘umefanya vyema’ saa ya hukumu,
Utumishi wa maserafi,
Imani ya waungamaji, neno la Mitume,
Sala za Mababu wa Imani, hati za kukunjwa za Manabii,
Matendo yote mema yaliyotendwa kwa ajili ya Bwana,
Na usafi wa nafsi za mabikira.
Leo najifungamanisha na
Nguvu za anga lenye nyota,
Mwanga unaotia uhai wa jua lenye fahari,
Weupe wa mwezi wakati wa jioni,
Kumweka kwa radi bila kizuizi,
Misukumo mikali ya upepo unaozunguka kwa tufani,
Ardhi iliyo imara, bahari yenye kina na chumvi,
Inayoyazunguka miamba ya kale ya kudumu milele.
Leo najifungamanisha na
Nguvu za Mungu za kunishikilia na kuniongoza,
Jicho Lake linilinde, uweza Wake unitegemeze,
Sikio Lake lisikilize hitaji langu.
Hekima ya Mungu wangu inifundishe,
Mkono Wake uniongoze, ngao Yake inikinge,
Neno la Mungu linijalie la kusema,
Jeshi Lake la mbinguni liwe mlinzi wangu.
Dhidi ya mitego ya dhambi ya mashetani,
Uovu unaolipa kishawishi nguvu,
Tamaa za maumbile zinazopigana ndani yangu,
Watu wenye uadui wanaoiharibu njia yangu;
Wawe wachache au wengi, mbali au karibu,
Kila mahali na kila saa,
Dhidi ya uadui wao mkali,
Najifungamanisha na nguvu hizi takatifu.
Dhidi ya uchawi na hila zote za Shetani,
Dhidi ya maneno ya uongo ya uzushi,
Dhidi ya maarifa yanayotia unajisi,
Dhidi ya ibada ya sanamu moyoni,
Dhidi ya ufundi mwovu wa mchawi,
Dhidi ya jeraha la kufisha na kuungua,
Wimbi linalokaba pumzi na mshale wenye sumu,
Unilinde, Kristo, hadi utakaporudi.
Kristo awe pamoja nami, Kristo ndani yangu,
Kristo nyuma yangu, Kristo mbele yangu,
Kristo kando yangu, Kristo anivute Kwake,
Kristo anifariji na kunihuisha.
Kristo chini yangu, Kristo juu yangu,
Kristo wakati wa utulivu, Kristo wakati wa hatari,
Kristo mioyoni mwa wote wanaonipenda,
Kristo kinywani mwa rafiki na mgeni.
Najifungamanisha na Jina,
Jina lenye nguvu la Utatu;
Kwa kulitia Jina hilo.
Watatu katika Mmoja, na Mmoja katika Watatu,
Ambaye kwa Yeye maumbile yote yameumbwa,
Baba wa milele, Roho, Neno:
Sifa kwa Bwana wa wokovu wangu,
Wokovu hutoka kwa Kristo Bwana.
Amina.
Picha kuu na Lawrence OP, Flickr
Zaidi kuhusu Mtakatifu Patriki>>>
