Kiswahili

Siku ya Thelathini na Nne – “Nina Kiu”


Toleo la Video

Baada ya hayo, Yesu, akijua kwamba sasa kila kitu kilikuwa kimetimizwa, ili Andiko litimie, alisema, “Nina kiu.” Palikuwa na chombo kilichojaa divai ya kawaida. Basi wakaweka sifongo iliyolowekwa katika divai kwenye kitawi cha hisopo, wakaifikisha mdomoni Mwake. Yohane 19:28-29

Mama yetu Mbarikiwa alipomsikia Mwana wake akisema maneno haya, “Nina kiu,” angetamani mara moja kuikata kiu Yake. Alizingatia kiu Yake ya kimwili, lakini alizingatia zaidi kiu Yake ya kiroho.

Askari alipochukua sifongo, akaichovya katika divai na kuiweka mdomoni Mwake, Mama yetu angepata faraja kiasi kutokana na tendo hili la fadhili. Lakini pia angeona maana kubwa katika tendo hili. Askari alikuwa ishara ya wanadamu walioanguka dhambini, na divai chachu ilikuwa ishara ya hali yetu ya kuvurugika. Lakini Yesu alitamani kutukomboa katika hali hiyo hiyo ya kuvurugika. Hakutamani “divai mpya” wala “maji safi ya chemchemi.” Aliwatamani wanadamu walioanguka dhambini. Alikuwa na kiu ya sisi kuja Kwake katika udhaifu na dhambi zetu. Mama yetu Mbarikiwa angetambua maana hii ya kina ya ishara hizo.

Yesu bado anapaza sauti leo, “Nina kiu!” Ana kiu nawe. Mara nyingi mno tunahisi kwamba tunaweza kuja Kwake kuikata kiu Yake ikiwa tu tunakuja tukiwa kama malaika. Mara nyingi mno tunaamini kwamba Yesu hututabasamia tu tunapokuja bila dhambi. Lakini hilo si kweli. Alikufa kifo cha kikatili namna hiyo ili tuweze kuja Kwake katika hali yetu ya kuvunjika. Tunamjia Kristo anayeteseka na mwenye kiu tukiwa na dhambi zetu na hali yetu ya kuvurugika. Sisi si divai mpya, bali ni divai chachu. Lakini tunapojiruhusu kuja kwa Bwana wetu katika hali hii, kiu Yake hukatika.

Nafsi yako iko katika hali gani? Je, unaona aibu kwa sababu ya dhambi zako? Je, unajifanya kuwa mtu mwingine ukidhani kwamba Yesu atakukubali tu ikiwa wewe ni mkamilifu? Hakuna jambo lililo mbali zaidi na ukweli kuliko hilo. Usisite kumjia Bwana wetu ukiwa na udhaifu, mahangaiko na dhambi zako zote. Usihofu atakachofikiri au kusema. Njoo Kwake. Ukimtumainia, tendo lako la unyenyekevu la kujitoa Kwake ukiwa mwenye dhambi litaiburudisha nafsi Yake.

Tafakari leo maneno hayo mawili matakatifu ya Bwana wetu aliyekuwa akifa: “Nina kiu.” Jua kwamba kiu Yake ni kwa ajili yako na kwamba anakutamani jinsi ulivyo. Mwendee, jikabidhi Kwake na umfurahishe. Mama yetu Mbarikiwa anatazama na kukungoja uitulize shauku iliyo ndani ya Moyo wa Mwana wake wa kimungu.

Mama yangu mpendwa sana, uliitambua na kuijali kiu ya kiroho iliyokuwa ndani ya Moyo wa Mwana wako. Pia ulitambua kwamba kiu Yake ilikuwa kwa ajili yangu na kwa ajili ya wanadamu wote. Uniombee ili niwe kama ile divai chachu, iliyoinuliwa hadi kwenye midomo ya Mwana wako wa kimungu.

Mama yangu mwenye upendo, uniombee ili niione dhambi yangu wala nisisite kumwendea Mwana wako nikiwa katika hali hii. Ninaomba niwe na ujasiri ninaouhitaji wa kuja nikiwa katika udhaifu wangu ili niutulize Moyo wa Mwana wako na Moyo wako mwenyewe Safi Kabisa.

Bwana wangu mwenye kiu, najua kwamba maneno Yako uliyoyasema kutoka Msalabani yalikuwa maneno ya kunialika niitulize shauku Yako ya kiroho. Unisaidie kutumaini kwamba unanipenda jinsi nilivyo. Unipe ujasiri ninaouhitaji wa kuitumainia huruma Yako na kukugeukia Wewe siku hii. Ninakupenda, Bwana mpendwa. Unisaidie nikupende zaidi.

Mama Maria, uniombee. Yesu, nakutumainia.

Siku ya Thelathini na Tano – “Imekwisha”

Yaliyomo


Pia Kinapatikana kama Kitabu cha Kielektroniki & Kitabu Chenye Jalada Laini!

Shiriki ukurasa huu: