
Basi mmoja wa wahalifu waliokuwa wametundikwa pale alimtukana Yesu, akisema, “Je, Wewe si Masihi? Jiokoe mwenyewe na sisi pia.” Lakini yule mwingine akamkemea, akamjibu, “Je, humwogopi Mungu, nawe umehukumiwa adhabu hiyohiyo? Nasi kwa kweli tumehukumiwa kwa haki, kwa kuwa adhabu tuliyopata inalingana na uhalifu wetu; lakini mtu huyu hajafanya tendo lolote la uhalifu.” Kisha akasema, “Yesu, unikumbuke utakapoingia katika ufalme Wako.” Akamjibu, “Amina, nakuambia, leo utakuwa pamoja nami Paradiso.” Luka 23:39-43
Mazungumzo haya kati ya Yesu na wale wahalifu wawili waliosulubiwa pamoja Naye, mmoja upande Wake wa kulia na mwingine upande Wake wa kushoto, yalikuwa na nguvu iliyoje! Mama yetu Mbarikiwa alisimama kimya, akiwasikiliza wakizungumza. Hapana shaka kwamba aliposikia maneno ya Mwanawe, moyo wake uliruka kwa furaha.
Tukio hili lina nguvu kubwa. Wale wahalifu wawili wanatuwakilisha sisi sote, ama upande wa kulia wa Yesu au upande Wake wa kushoto. Kila mmoja wetu humwambia Yesu maneno kama hayo. Kila mmoja wetu atakabiliwa na ukimya wa Bwana wetu au atamsikia akisema, “Leo utakuwa pamoja nami Paradiso.”
Ni mhalifu yupi anayekuwakilisha kwa usahihi zaidi? Mhalifu mmoja amejaa hali ya kujiona mwenye haki inayotokana na kiburi. Yule mwingine amejaa huzuni inayotokana na unyenyekevu. Wote wawili wana hatia, lakini ni mmoja tu anayesamehewa. Wote wawili wanamtambua Yesu kuwa ndiye Masihi, lakini ni mmoja tu anayekubali kuwajibika kwa dhambi yake.
Mhalifu wa kwanza anasema, “Jiokoe mwenyewe na utuokoe sisi.” Asichokiona ni kwamba Yesu yuko katika harakati za kufanya jambo hilo hilo. Kwa kuteseka na kufa, Yeye anaangamiza dhambi na kuwapatia wokovu wote wanaotafuta huruma Yake kwa unyenyekevu. Kifo Chake ndicho lango la kuingia Paradiso. Mhalifu wa kwanza haoni jambo hili. Badala yake, anatafuta “wokovu” wa kidunia wa papo hapo kwa kumtaka Yesu athibitishe uwezo Wake kwa kumwokoa kutoka katika kifo cha msalabani.
Lakini yule mhalifu mwingine anaitambua kazi tukufu ya Bwana wetu. Anakiri kwamba kifo chake mwenyewe ni utekelezaji wa haki kutokana na dhambi zake. “Sisi tumehukumiwa kwa haki,” anakiri. Lakini huyo “mnyang’anyi mwema” haishii hapo. Kwa unyenyekevu anamwomba Yesu amkumbuke atakapoingia katika Ufalme Wake. Yesu anakubali na kumpa mhalifu huyu neema inayopatikana kwa kifo cha Yesu mwenyewe kilichokaribia, naye anamwahidi Paradiso.
Mama yetu Mbarikiwa alipokuwa akitazama, moyo wake ulijaa furaha na huzuni. Huzuni yake ilitokana na mhalifu wa kwanza ambaye hakukiri hatia yake kwa unyenyekevu. Furaha yake ilitokana na yule mhalifu mwingine aliyejinyenyekeza mbele ya Mwanawe na kupokea uzima wa milele. Mwanawe alipokuwa ametundikwa Msalabani, Mama Maria aliona jinsi ahadi ya Paradiso ilivyoombwa na kisha kutolewa. Furaha aliyohisi kwa kushuhudia wokovu wa mhalifu huyu ilimfariji katika huzuni aliyohisi kwa sababu ya ukatili aliotendewa Mwanawe.
Sote tumeitwa kuuletea furaha moyo wa Mama yetu Mbarikiwa. Tunafanya hivyo tunapokiri kwa unyenyekevu kwamba sisi pia ni “wahalifu” kwa maana ya kwamba sisi ni wenye dhambi. Adhabu tunayostahili ni kifo. Lakini tukikiri ukweli huu kwa unyenyekevu, lazima pia tujipatie ujasiri wa kumsihi Bwana wetu atuhurumie na kutukaribisha Paradiso.
Tafakari leo maneno ya huyu mnyang’anyi mwema. “Yesu, unikumbuke utakapoingia katika ufalme wako.” Bwana wetu alikufa ili kuifungua milango ya Paradiso iliyokuwa imefungwa hapo mwanzo kwa dhambi ya Adamu. Tafakari pia furaha unayomletea Mama yetu Mbarikiwa kila unapojinyenyekeza mbele ya neema iliyopatikana kwa Msalaba wa Mwanawe.
Mama mpendwa sana, uliposimama mbele ya Mwanao na kumsikia akimwahidi wokovu yule mnyang’anyi aliyetubu, moyo wako uliruka kwa furaha safi. Ninaomba kwamba mimi pia niweze kuuletea furaha moyo wako unapoona neema ya Msalaba wa Mwanao ikimiminika juu yangu.
Mama yangu mpendwa, uniombee ili mimi pia nifurahie toba ya wenye dhambi wote. Mara nyingi mno ninajikuta nikiwahukumu wengine na nikisita kusamehe. Moyo wangu na uige upendo wako safi, nami nipate furaha katika kuongoka kwa wote wanaomgeukia Mwanao.
Mwokozi wangu mwenye kusamehe, nimehukumiwa kwa haki kwa sababu ya dhambi zangu, nami ninastahili kifo. Unisamehe na kunihurumia, Bwana mpendwa. Ninatubu dhambi zangu na kukuomba Wewe neema ya kukumbukwa Nawe katika Ufalme Wako mtukufu.
Mama Maria, uniombee. Yesu, nakutumainia.
Siku ya Thelathini na Mbili – “Mwanamke, Tazama Mwanao…Tazama Mama Yako”
Pia Kinapatikana kama Kitabu cha Kielektroniki & Kitabu Chenye Jalada Laini!

