Kiswahili

Siku ya Pili – Nguvu ya Moyo Safi

Toleo la Video

Karibu na msalaba wa Yesu walikuwa wamesimama mama yake na dada ya mama yake, Maria mke wa Klopa, na Maria wa Magdala. Yohane 19:25

Leo, kwa mara nyingine, tunalitazama tukio hili takatifu sana la Mama wa Yesu akiwa amesimama chini ya Msalaba. Zingatia kwamba Injili ya Yohane inasema alikuwa “amesimama.”

Hakuna shaka kubwa kwamba hisia za kibinadamu alizokuwa nazo Mama Maria zilikuwa kali sana na nzito. Moyo wake ulivunjika na kuchomwa alipokuwa akimtazama Mwanawe mpendwa akining’inia Msalabani. Lakini alipokuwa akimtazama, aliendelea kusimama.

Kusimama kwake kuna maana kubwa. Ni njia ndogo na isiyo ya wazi sana ambayo kifungu hiki cha Injili kinatumia kuonyesha nguvu zake katikati ya uchungu mkubwa aliokuwa nao. Hakuna jambo ambalo lingeweza kumvunja moyo zaidi kuliko kushuhudia ukatili wa namna hiyo ukitendwa kwa yule aliyempenda kwa moyo wake wote. Hata hivyo, katikati ya uchungu huu mkali sana, hakujiachilia kulemewa na huzuni wala kukata tamaa. Aliendelea kusimama, kwa nguvu zote, akiudhihirisha kwa uaminifu upendo wa mama hadi mwisho.

Nguvu za Mama yetu Mbarikiwa chini ya Msalaba zinatokana na moyo usio na doa kwa namna yoyote ile. Moyo wake haukuwa na doa katika upendo, ulikuwa imara kabisa, mwaminifu kabisa, thabiti katika azimio lake, na ulijaa matumaini yasiyofifia katikati ya machafuko ya dunia. Kwa mtazamo wa ulimwengu, Mwanawe alikuwa akipatwa na janga kubwa kuliko yote yanayoweza kutokea. Lakini kwa mtazamo wa Mbinguni, wakati huohuo alikuwa akialikwa kuudhihirisha upendo safi wa Moyo wake Usio na Doa.

Ni moyo uliopenda kwa ukamilifu tu ambao ungeweza kuwa imara kiasi hicho. Hasa matumaini ambayo yangekuwa hai ndani ya moyo wake yalikuwa ya kustaajabisha na yenye utukufu. Mtu anawezaje kuwa na matumaini na nguvu kama hizi anapokabiliwa na uchungu wa namna hiyo? Kuna njia moja tu, nayo ni njia ya upendo. Upendo safi na mtakatifu katika Moyo Usio na Doa wa Mama yetu Mbarikiwa ulikuwa mkamilifu.

Tafakari leo juu ya nguvu za moyo wa Mama yetu Mbarikiwa. Uutazame upendo aliokuwa nao kwa Mwanawe, na uache moyo wako uvutiwe na kuustaajabia upendo huu safi na mtakatifu. Unapoona uchungu maishani mwako ukiwa mkali na kukulemea, ukumbuke upendo ulio katika Moyo wa mama huyu. Sali ili moyo wake uutie msukumo moyo wako na nguvu zake ziwe nguvu zako unapojitahidi kukabiliana na misalaba na magumu ya maisha.

Mama yangu mwenye upendo mkuu, nivute niingie katika usafi na nguvu za moyo wako. Ulisimama chini ya Msalaba, ukimtazama Mwanao alipokuwa akitendewa ukatili mkubwa namna ile. Nikaribishe ndani ya moyo wako wenye upendo mkamilifu, ili nipate kuhamasishwa nawe na kuimarishwa na ushuhuda wako wenye utukufu.

Mama yangu mpendwa, uliposimama chini ya Msalaba, ulikuwa mfano kwa watu wote. Hakuna mahali bora pa kuwa kuliko chini ya Msalaba. Nisaidie nisiugeuzie Msalaba mgongo kamwe, nikijificha kwa hofu, maumivu au kukata tamaa. Nikomboe kutoka katika udhaifu wangu na uniombee ili niweze kuiga nguvu ya upendo wa moyo wako.

Bwana wangu wa thamani, ulipokuwa ukining’inia Msalabani, uliruhusu upendo wa Moyo Wako uungane na moyo wa mama Yako. Nikaribishe katika upendo huu mnaoshirikiana, ili nami niungane Nawe katika maumivu na mateso Yako. Nisikuondolee macho yangu kamwe, Bwana mpendwa.

Mama Maria, utuombee. Yesu, nakutumainia.

Siku ya Tatu – Mawazo ya Mama wa Mungu

Yaliyomo

Inapatikana kama Kitabu cha Kielektroniki & Kitabu chenye Jalada Laini!

Shiriki ukurasa huu: