Kiswahili

Siku ya Kumi na Nane – “Huu ni Mwili Wangu…Hii ni Damu Yangu”

Toleo la Video

Walipokuwa wakila, Yesu alitwaa mkate, akatamka baraka, akaumega, akawapa wanafunzi wake akisema, “Twaeni mle; huu ndio mwili wangu.” Kisha akatwaa kikombe, akashukuru, akawapa akisema, “Nyweni kutoka humo ninyi nyote, kwa maana hii ndiyo damu yangu ya agano, itakayomwagwa kwa ajili ya wengi ili kusamehe dhambi.” Mathayo 26:26-28

Adhimisho la kwanza la Ekaristi Takatifu Sana lilifanyika katika Karamu ya Mwisho, Yesu alipoanzisha Ukuhani na Ekaristi Takatifu mbele ya Mitume Wake. Utoaji wa Sadaka hii ya kiibada ulifikia kilele katika sadaka Yake ya kimwili Msalabani, alipokunywa divai chungu na kupaaza sauti, “Imekwisha!” Mama yetu Mbarikiwa alishuhudia kujimimina huku kwa milele alipokuwa amesimama chini ya Msalaba. Akiwa hapo, alikiabudu kila tone la Damu Yake Azizi lililoanguka ardhini ili kuutakatifuza ulimwengu.

Baada ya Ufufuko, Mama yetu Mbarikiwa alijaliwa kushiriki uzima wa Mwanawe kwa namna mpya na ya kina, kila aliposhiriki karamu ya Ekaristi Takatifu. Aliinywa Damu Azizi ya Mwanawe mwenyewe na kuula Mwili Wake Mtakatifu alipojiunga na Mitume katika Misa Takatifu.

Taswira ya mateso na kifo cha Mwana wake ilikuwa imejikita milele katika akili yake na kuchapishwa moyoni mwake. Lakini muungano wake Naye kwa njia ya kupokea Komunyo Takatifu ulimwezesha kuyaelewa kikamilifu mateso na kifo Chake. Kila alipopokea Mwili na Damu Yake, alipokea pia Roho na Umungu Wake. Katika zawadi hii ya Ekaristi, alionja ukaribu Wake kwa namna ambayo hakuwahi kuionja hapo awali, naye alijua kwamba kifo Chake Msalabani kilikuwa chemchemi ya muungano wake mpya na wa kina Naye. Hakuwa tena yule ambaye alimtazama kwa upendo akiwa mbali. Hakuwa tena yule ambaye alimbeba tumboni mwake tu. Sasa alikuwa yule ambaye alimpokea kama chakula, na kwa njia hiyo aliingia ndani ya moyo na roho yake kwa namna ya kina kabisa.

Alipomtazama na kumwona akikata roho, matumaini yote ya kidunia ya kuwa Naye yalipotea. Lakini katika wakati huo, alipolia kwa sauti, “Imetimia!”, uhusiano wake na Mwana wake ulibadilika milele. Uhai Wake ulikuwa umerudishwa kwa Mungu Baba, lakini yeye alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kumpokea katika Ekaristi Takatifu.

Tafakari leo juu ya uhusiano wa kina ambao Mama yetu Mbarikiwa alikuwa nao na Mwana wake. Ushirika wake na Yesu ulifikia kiwango kipya na cha kina zaidi cha upendo alipojaliwa kumpokea katika mwili na roho yake katika Ekaristi Takatifu. Sisi pia sote tumeitwa kuwa na ushirika wa kina namna hiyo na Yesu. Sisi pia sote tunaalikwa kuwa kitu kimoja Naye tunaposhiriki zawadi ya Misa Takatifu. Tafakari jinsi unavyoamini kwa kina uwepo wa Bwana wetu katika Sakramenti hii. Tafakari jinsi unavyojifungua kikamilifu kupokea neema za Zawadi hii. Jitoe upya ili ume me zwe na Bwana wetu unapopokea Mwili na Damu, Roho na Umungu Wake. Jua kwamba muungano unaoitwa kuishi Naye unatokana na zawadi Yake tukufu ya Msalaba.

Mama yangu mwenye upendo, ulipomtazama Mwana wako ulimwona akikata roho. Ulimtazama akifa na kuutoa uhai Wake kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu. Lakini uliona pia mengi zaidi. Ulipoiona sadaka Yake ikifikia utimilifu, uliiona pia ikibadilika na kuwa mwanzo mpya. Ulishuhudia mwanzo wa Ekaristi Takatifu Sana, ambayo ulijaliwa kuishiriki kwa muda wote uliobaki wa maisha yako.

Mama yangu mpendwa, uniombee nipate neema ya kushiriki kwa uaminifu katika kuupokea Mwili na Damu ya Mwana wako. Nami, kama wewe, nimpokee kwa imani iliyo kuu kabisa na kuiruhusu Sadaka Yake ya wokovu ienee katika kila sehemu ya roho yangu.

Bwana wangu mpendwa, ulitupatia Ekaristi kama zawadi ya uwepo Wako wa daima kati yetu. Katika zawadi hii yenye thamani, unanialika kuingia katika ushirika wa kina Nawe. Ninapoutazama Msalaba Wako na kuiona Damu Yako ikimwagika, nisaidie kuifungua roho yangu kama sifongo linalofyonza uwepo Wako wa kimungu. Jiunge nami, Bwana mpendwa, ninapojitoa Kwako.

Mama Maria, uniombee. Yesu, nakutumainia.

Inayofuata: Siku ya Kumi na Tisa – Mahangaiko Bustanini

Yaliyomo

Inapatikana kama Kitabu cha Kielektroniki & Kitabu chenye Jalada Laini!

Shiriki ukurasa huu: