Kiswahili

Utangulizi

Kwaresima ni kipindi kitakatifu cha mwaka. Kwa nje, wengi husita wanapofikiria kwamba Kwaresima inakaribia, lakini ndani kabisa ya mioyo yao, Wakristo waaminifu hukingojea kipindi hiki kitakatifu kwa matumaini kwamba kitazaa matunda mema maishani mwao.

Maisha ya Yesu yalikuwa na sadaka na mateso, ambayo kwayo alitujalia upendo Wake mkamilifu. Hatutaweza kamwe kuielewa kikamilifu roho Yake ya kimungu, hata Mbinguni. Utatu Mtakatifu pekee ndio unaouona utimilifu wa kila Nafsi ya kimungu. Hata hivyo, tunapaswa kujitahidi kuyaelewa maisha ya kibinadamu ya Bwana wetu ili tuweze kushiriki maisha Yake, kumwiga, na kupokea thawabu za milele anazotamani kuwajalia wale wanaompenda.

Kumbuka maneno ya Yesu, “Ingieni kwa kupitia lango jembamba; kwa maana lango ni pana na njia ni pana iendayo kwenye maangamizi, nao waingiao humo ni wengi. Jinsi lilivyo jembamba lango na jinsi ilivyobana njia iendayo uzimani. Nao waionao ni wachache” (Mathayo 7:13–14). Kuingia kwa kupitia “lango jembamba” hilo ni njia inayohitaji azimio thabiti na upendo wa kujitoa sadaka. Ili kuifuata njia hiyo iliyobana na yenye changamoto, ni lazima tukabiliane na mambo magumu ya maisha yetu, yakiwemo dhambi zetu.

Kuzikabili dhambi zetu kunahitaji unyofu na unyenyekevu wa kina. Ni rahisi kujitetea kwa visingizio kana kwamba dhambi si dhambi, na kujichukulia kwamba Mungu, kwa huruma Yake, atasamehe daima. Mungu hutujalia msamaha—lakini kwa sharti kwamba tuzikabili dhambi zetu, tuzitubie, na tujitahidi kurekebisha maisha yetu. Hili si jambo dogo.

Zaidi ya hayo, kadiri tunavyomkaribia Mungu, ndivyo tutakavyoona kwa uwazi zaidi yote ambayo hatukuyaona hapo awali. Dhambi huonekana wazi zaidi kadiri hata mapungufu madogo kabisa yanavyofunuliwa nuruni. Kufikia kiwango hiki cha umakini kunahitaji bidii kubwa, sala, na moyo ulio wazi.

Kwa kuwa Kwaresima ndio wakati muhimu zaidi wa mwaka wa kutafakari dhambi zetu, tenga muda wa kuyatazama mapungufu yako mwenyewe kwa mitazamo mbalimbali. Usivunjike moyo unapofanya hivyo. Tafakari dhambi ukiwa na matumaini ya kuwekwa huru kutoka katika dhambi hizo. Lakini hutaupata kamwe uhuru huo usipoichunguza nafsi yako kwa unyofu, kwa kina, na bila kukoma, kwa mtazamo wa Mungu. Ikiwa unatamani maisha ya utakatifu wa kweli, mchakato huu unaweza kuonekana wenye kuchosha. Hata hivyo, kuchosha si sawa na kuwa na wasiwasi wa kupindukia kuhusu dhambi. Wasiwasi huo ni hali ya kujichunguza kuhusu dhambi bila kukoma, bila imani wala matumaini katika huruma ya Mungu isiyo na mwisho. Huruma Yake inapokuwa sehemu ya mchakato huo, kuondoa kwa sala hata dhambi ndogo kabisa maishani mwako huwa furaha kubwa na njia ya kuelekea uhuru wa ajabu.

Kwaresima hufikia mwisho wakati wa kuanza kwa kipindi cha Pasaka. Ni muhimu kuikumbuka Pasaka unapopitia Kwaresima, unapotoa sadaka, unapochunguza dhamiri yako, na kuungama dhambi zako. Sadaka, mateso, na kifo huvunja moyo ikiwa si njia ya kufikia lengo kubwa zaidi, nalo ni Ufufuko wa Kristo na ushiriki wako katika maisha Yake mapya.

Kitabu hiki kinatoa tafakari za kipindi cha Kwaresima zinazotokana na siku arobaini za Yesu jangwani. Aidha, zitatolewa tafakari kuhusu Injili za Jumapili, dhambi kuu saba, na Juma Takatifu. Kwa kuwa Kwaresima ina zaidi ya siku arobaini Jumapili zinapohesabiwa, kitabu hiki kitatoa tafakari tofauti kwa kila Jumapili ya Kwaresima, na kuziacha siku nyingine, hadi Jumamosi Kuu, zitimize siku arobaini za kimapokeo.

Bwana akujalie Kwaresima yenye kuzaa matunda na kukubadilisha unaposafiri pamoja Naye katika siku Zake arobaini jangwani, katika mahubiri na miujiza Yake, na katika Mateso Yake matakatifu.

Bwana wa matumaini yote, ninapoanza kipindi hiki kitakatifu cha Kwaresima, ninaomba unibadilishe, unigeuze, na kunifunulia yote unayotaka kunijulisha. Ninajifungua kwa mapenzi Yako matakatifu kwa kadiri niwezavyo, na kuitegemea neema Yako ikamilishe yaliyobaki. Nisaidie kuyachunguza maisha yangu kwa unyenyekevu na unyofu ili nitakaswe dhambi zangu na kuiga kwa ukamilifu zaidi upendo Wako wa kujitoa sadaka. Nivute nishiriki Mateso na kifo Chako, Bwana mpendwa, ili niweze kushiriki utukufu wa Ufufuko Wako. Yesu, Masihi na Mfalme, nakutumainia!

Yaliyomo

Shiriki ukurasa huu: