Kiswahili

Kipindi cha Noeli

Njia Imeandaliwa…Je, Uko Tayari?

Januari 2, inapokuwa kabla ya Epifania

Yohane alisema: “Mimi ni sauti ya mtu anayepaaza sauti jangwani, ‘Inyosheni njia ya Bwana,’ kama alivyosema nabii Isaya.” Yohane 1:23

Yohane Mbatizaji yu hai!  Ndiyo, yu hai Mbinguni, akipokea tuzo yake ya milele.  Lakini pia yu hai kwa namna nyingine.  Yu hai katika tangazo lake linaloendelea, akituita tutubu na kutuita tumwandaliye Bwana njia katika maisha yetu.

Ujumbe wake una umuhimu uleule kwetu leo kama ulivyokuwa miaka ipatayo 2,000 iliyopita. Alipokuwa akiishi duniani, alihubiri ili kuandaa njia moja kwa moja kwa ajili ya Kristo. Aliandaa njia ili Masiya aingie kimwili katika ulimwengu wetu na kutupatia zawadi ya wokovu wa milele. Lakini Mtakatifu Yohane anaendelea kuandaa njia ya Bwana, ikiwa tuko tayari kusikiliza.

Tunajifunza kutoka kwa Mtakatifu Yohane kwamba hatua ya kwanza kuelekea maisha ya utakatifu ni “kuinyosha njia ya Bwana.” Tunafanyaje hivyo? Tunainyoshaje njia ya Bwana? Tunafanya hivyo kwa kukiri kwa unyenyekevu dhambi zile zinazomzuia Yesu kuja kwetu na kuyabadilisha maisha yetu.

Tafakari leo kuhusu mwaka uliopita na pia mwaka unaokuja.  Ni nini unachohitaji kuachilia kutoka katika yaliyopita, na ni nini unachohitaji kukizingatia katika mwaka unaokuja?  Weka azimio lililo wazi la kutambua kizuizi chochote kinachozuia ujio wa Kristo moyoni mwako, na ujiruhusu kuyagundua maisha mapya yanayokungoja mwaka huu unaokuja.

Bwana, ulikuja ulimwenguni humu kwa upendo Wako mkamilifu kwangu. Ulikuja kuniokoa kutoka katika dhambi zote na kunikomboa kutoka katika uovu wote. Nisaidie kuona kile kilichonitenga Nawe katika mwaka huu uliopita na kukukabidhi hicho. Nisaidie pia kuwa na matumaini na kuona yaliyo mbele yangu na yote unayoniitia. Na niyazingatie maneno ya Mbatizaji na kuinyoosha njia iliyo mbele yangu ili niweze kufuata mapenzi Yako makamilifu. Yesu, nakutumainia.


Tazama, Mwanakondoo wa Mungu

Tarehe 3 Januari, inapokuwa kabla ya Epifania

“Tazama Mwanakondoo wa Mungu, anayeondoa dhambi ya ulimwengu.” Yohane 1:29b

Maneno haya tunayoyafahamu ya Mtakatifu Yohane Mbatizaji yanatupatia tafakari nzuri. Husemwa kila tunapohudhuria Misa Takatifu wakati padre anapoinua Hostia Takatifu. Maneno haya, yaliyosemwa kwanza na Mtakatifu Yohane Yesu alipomjia ili abatizwe, ni maneno tunayoweza kuyatafakari kwa sala katika maisha yetu yote.

Fikiria kauli hiyo: “Tazama Mwanakondoo wa Mungu…”  Ni vizuri kuanza kwa kumwazia Yohane akisema maneno haya kumhusu Yesu.  Lakini kuanzia hapo, tunayatumia kwa Ekaristi na kwa nyakati nyingine zisizohesabika katika maisha yetu ya kila siku.

Yohane aliposema maneno haya kwa mara ya kwanza, “Mwanakondoo wa Mungu” alionekana kwa namna ya kawaida sana.  Macho ya wote waliokuwapo yalimwona tu mtu wa kawaida akija mahali hapo.  Lakini macho ya imani yalimwona Yeye ambaye angeutoa uhai Wake kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu kama Mwanakondoo wa Sadaka.

Na tunapoitazama Hostia Takatifu, inapoinuliwa katika Misa Takatifu ili wote waione, tunamwona Yesu, Mwanakondoo wa Sadaka, kwa namna iliyofichika hata zaidi.  Kwa macho yetu, tunaona kipande cha mkate.  Lakini kwa macho ya imani, kwa mara nyingine tunamtazama Mwokozi.

Mwanakondoo wa Mungu anayetolewa sadaka huendelea kutujia katika siku yetu nzima.  Yuko kila mahali kutuzunguka, akitujia kwa namna iliyofichika, akijifunua kupitia imani.  Je, unamwona?  Leo unaitwaje kuutazama uwepo Wake wa kimungu na wa kujitoa sadaka?  Yukoje katika matendo ya upendo usio na ubinafsi?  Anakujiaje kila siku, na anatamani umpelekeje kwa wengine kila siku?

Tafakari leo kuhusu maneno hayo matakatifu.  “Tazama Mwanakondoo wa Mungu.”  Mtafute, ukitarajia kwamba uwepo Wake wa kimungu umefichika lakini ni halisi.  Mgundue kwa macho ya imani na ufurahi anapokukaribia.

Bwana, nautazama uwepo Wako wa kimungu leo na kila siku.  Nakutafuta na kukupenda.  Nipe macho ya imani ili niugundue uwepo Wako halisi lakini uliofichika nyakati zote.  Uko kila mahali kunizunguka kila siku.  Nisaidie kufurahia jinsi ulivyo karibu nami daima.  Yesu, nakutumainia.


Kuwaelekeza Wengine kwa Yesu

Tarehe 4 Januari, inapokuwa kabla ya Epifania

Yohane alikuwa amesimama pamoja na wanafunzi wake wawili, naye alipomwona Yesu akipita, alisema, “Tazama, Mwanakondoo wa Mungu.” Wale wanafunzi wawili walisikia alichosema, wakamfuata Yesu. Yohane 1:35–37

Fikiria kama Yohane angefurahia sana jinsi kila mtu alivyokuwa akimzingatia kiasi cha kuamua kuendelea kuwavutia watu kwake mwenyewe.  Fikiria kama angeamua kwamba angeweza kuwa “mfalme” ikiwa angetumia fursa zake kwa ujanja.  Fikiria kama angejishughulisha sana na umaarufu wake mwenyewe kiasi kwamba asingetaka kuwaelekeza wengine kwa Yesu na kuhatarisha kuwapoteza kwao kumfuata Yeye.  Bila shaka, sivyo ilivyotokea.  Kilichotokea ni kwamba Yohane alitimiza jukumu lake vizuri sana, akimwandalia Yesu njia na kuwaelekeza wengine Kwake wakati ufaao ulipofika.

Katika kifungu hiki hapo juu, Yohane anawaelekeza wafuasi wake wawili wamtazame Bwana wetu. Anawaambia, “Tazama, Mwanakondoo wa Mungu…” Wanamwona Yesu na kumwacha Yohane.

Huenda jambo hilo lilimletea Yohane furaha iliyochanganyika na uchungu. Huenda kwa namna fulani alihisi uchungu wa kuwapoteza wafuasi wake. Lakini uchungu wowote wa kuwapoteza ungebadilishwa na kupunguzwa na furaha ya kujua kwamba alikuwa akitimiza kusudi la maisha yake kwa kuwaelekeza wengine kwa Kristo.

Ndivyo inavyopaswa kuwa kwetu pia. Ni rahisi kujishughulisha na mambo yetu wenyewe tu maishani. Ni rahisi kutaka watu wote watuelekezee sisi fikira zao na, tunapopata uangalifu huo, ni vigumu kuuachilia. Lakini upendo wa kweli wa Kikristo daima hauna ubinafsi. Daima humwelekea Bwana wetu na daima huwaelekeza wengine kwa Yesu. Yohane alituwekea mfano mzuri sana wa maisha haya ya fadhila; nasi tumeitwa kufanya vivyo hivyo.

Tafakari leo kuhusu watu walio katika maisha yako. Je, unatafuta uangalifu wao kwa ajili ya masilahi yako ya kibinafsi? Au unafurahia nafasi nyingi ulizo nazo za kuwaelekeza kwa Yesu? Kwa kuwaelekeza wengine kwa Bwana wetu, utapata utoshelevu unaozidi chochote ambacho ubinafsi ungeweza kukupa, nawe utathawabishwa kupita kiasi.

Bwana, nisaidie kutafuta daima njia za kuwaelekeza Kwako watu walio katika maisha yangu. Nisaidie kutokuwa na ubinafsi na kujitoa sadaka nyakati zote. Nisaidie kutambua kwamba upendo unakuhusu Wewe kabisa na unahusu kabisa kuwasaidia wengine wakujue na kukufuata. Hilo linaponihitaji kujitoa sadaka, nisaidie kuipokea sadaka hiyo kwa furaha na bidii ya moyo wote. Yesu, nakutumainia.


Kuwa Wewe Mwenyewe

Januari 5, inapokuwa kabla ya Epifania

Yesu alimwona Nathanaeli akimjia, akasema juu yake, “Huyu hapa ni Mwisraeli wa kweli. Hamna unafiki ndani yake.” Nathanaeli akamwambia, “Unanijuaje?” Yesu akamjibu, akamwambia, “Kabla Filipo hajakuita, nilikuona chini ya mtini.” Nathanaeli akamjibu, “Rabi, Wewe ndiwe Mwana wa Mungu; Wewe ndiwe Mfalme wa Israeli.” Yohane 1:47–49

Je, kweli Nathanaeli alifikia kumjua na kumkiri Kristo kuwa Mwana wa Mungu na Mfalme wa Israeli kwa sababu tu Yesu alimwambia kwamba alimwona chini ya mtini? Inaonekana hivyo. Lakini ni wazi kwamba kuna mengi zaidi yanayotendeka hapa.

Kwanza kabisa, ni muhimu kuangalia maneno ya kwanza ya Yesu kuhusu Nathanaeli. Yesu anasema kwamba “Hamna unafiki ndani yake.” Kwa maneno mengine, Nathanaeli alikuwa mtu mwaminifu, mkweli, mnyofu wa moyo na asiye na hila. Alivyoonekana kwa nje ndivyo alivyokuwa kwa ndani. Ni sifa nzuri iliyoje!

Pili, tunaweza kuona kwamba unyofu huu unamwongoza Nathanaeli kuikiri imani yake katika Kristo karibu mara moja. Inawezekanaje hivyo? Je, ni jambo fulani ambalo Yesu alisema? Ni wazi kwamba jambo lenye kina zaidi ndilo lililomwongoza Nathanaeli kuikiri imani yake katika Kristo. Ilikuwa zawadi ya kiroho ya imani ambayo kwa njia yake Roho Mtakatifu alimfunulia jambo hili. Jambo jema ni kwamba Nathanaeli, akiwa mtu asiye na hila, alimsikiliza Roho Mtakatifu akisema moyoni mwake, kisha akatamka usadikisho huu waziwazi na bila kuficha chochote. Ni sifa nzuri ajabu kuwa nayo wakati mtu yuko pia tayari kuupokea ukweli.

Katika maisha yetu wenyewe tunahitaji kuiga sifa hii ya Nathanaeli. Ni lazima tuwe tayari kumsikiliza Roho Mtakatifu akisema nasi, kisha tuwe na ujasiri na uaminifu katika misimamo iliyowekwa mioyoni mwetu ili tuweze kuifunua kwa wengine kwa uaminifu na waziwazi. Kwa kuiga sifa hizi, sisi pia tutaweza kutumika kama vyombo vya Bwana wetu kwa wote tunaokutana nao.

Tafakari leo kuhusu mkutano huu unaovutia kati ya Yesu na Nathanaeli. Uko tayari kwa kiasi gani kuisikiliza sauti ya Mungu ikisema katika dhamiri yako? Na uko tayari kwa kiasi gani kushirikisha wengine zawadi yako ya imani waziwazi na kwa uaminifu? Jitoe kuwa chombo kilicho tayari kuifikisha sauti ya Mungu katika ulimwengu huu, ukimwiga Mtume huyu mkuu.

Bwana, ninatamani kuisikia na kuitambua sauti Yako ikisema nami katika dhamiri yangu. Ninapokusikia, nisaidie kuwa tayari na kuwa na nia ya kukufunua kwa wengine. Yesu, nakutumainia.


Hadhi ya Mtoto wa Mungu

Januari 6, inapokuwa kabla ya Epifania

“Wewe ndiwe Mwanangu mpendwa; nimependezwa Nawe sana.” Marko 1:11b

Maneno haya, yaliyosemwa na Baba wa Mbinguni wakati wa ubatizo wa Yesu, hayafunui tu hadhi ya Mwana wa Mungu, bali pia yanafunua mengi kutuhusu sisi. Ni maneno yanayosemwa kumhusu kila mmoja wetu kutokana na ubatizo wetu wenyewe katika Kristo.

Wewe ni nani? Hili ni swali muhimu. Mara nyingi sana tunajitambulisha kwa kitu kingine badala ya ukweli. Mara nyingi tunaweza kujitambulisha kwa yale tunayoyatimiza au tunayoshindwa kuyatimiza. Na kwa kufanya hivyo, tunaelekea kuruhusu matendo yetu yaamue hadhi yetu.

Ingawa ni kweli kwamba matendo yetu ama yanapatana na hadhi yetu au yanapingana nayo, si kweli kwamba matendo yetu ndiyo yanayoamua hadhi yetu. Hadhi yetu inaamuliwa na jambo moja: Ubatizo. Katika Ubatizo wetu tunafanywa kuwa wana na binti za Baba wa Mbinguni. Kwa hiyo, Baba anatuona kuwa watoto Wake wapendwa na kututazama kwa furaha kubwa. Si kwa sababu ya yale tunayofanya au tusiyofanya, bali kwa sababu ya sisi tulivyo.

Tafakari leo kuhusu maneno haya yaliyosemwa na Baba, na ukubali yaelekezwe kwako. “WEWE ni mtoto wangu mpendwa,” asema Baba wa Mbinguni. “Nimependezwa na WEWE.” Baba amependezwa nawe kwa sababu unamfurahisha kwa kuwa tu mtoto Wake. Tafakari ukweli huo na uuache uzame moyoni mwako tunapojiandaa kwa adhimisho lijalo la Ubatizo wa Bwana.

Bwana, nisaidie daima kutambua hadhi yangu kama mtoto Wako. Nisaidie kujua na kuamini kwamba hakuna jambo ninaloweza kufanya ili kuongeza au kupunguza upendo Wako kwangu, wala hadhi ninayopokea kutokana na upendo Wako. Nisaidie daima kutambua kwamba maisha yangu yanakuletea furaha kubwa, si kwa sababu ya ninayofanya au nisiyofanya, bali kwa sababu ya mimi ni nani. Nakushukuru kwa kunipenda kama Baba mkamilifu. Tafadhali, nisaidie daima kuujua na kuupokea upendo huu mkamilifu. Yesu, nakutumainia.


Udhihirisho wa Furaha

Januari 7, inapokuwa kabla ya Epifania

Msimamizi wa karamu alimwita bwana arusi na kumwambia, “Kila mtu hutoa divai nzuri kwanza, kisha watu wakiisha kunywa kwa wingi, hutoa iliyo duni; lakini wewe umeihifadhi divai nzuri mpaka sasa.” Yesu alifanya hili kuwa mwanzo wa ishara zake huko Kana ya Galilaya, na hivyo akaudhihirisha utukufu wake, nao wanafunzi wake wakaanza kumwamini. Yohane 2:9c–11

Katika Injili ya Yohane kuna “ishara” saba anazofanya Yesu zinazodhihirisha nguvu na utukufu Wake. Ishara hii, iliyo ya kwanza kati ya ishara Zake, inatufunulia mengi. Kama simulizi linavyoeleza, divai katika arusi ya Kana inaisha, Mama wa Yesu anawaombea kwa Mwanawe, naye anawaambia watumishi wajaze maji katika mitungi sita ya mawe, na mara moja maji hayo yanageuzwa kuwa divai. Wala si divai ya kawaida! Ni divai bora kabisa.

Divai ni ishara ya wingi usio na kipimo wa Mungu. Inadhihirisha shangwe na furaha ya kweli. Yesu, kwa kuwapa divai bora kwa wingi, anadhihirisha kwamba amekuja kutujaza furaha kamilifu kabisa kwa wingi.

Baadaye divai pia ilitumika kama njia ya kutupatia Damu Azizi ambayo Yesu angeimwaga kwa ondoleo la dhambi. Tunaipokea zawadi hii tele kila tunapopokea Komunyo Takatifu.

Tunapokaribia mwisho wa kipindi cha Krismasi na mwanzo wa Kipindi cha Kawaida, ruhusu ishara hii ya kwanza ya kimiujiza ya Yesu iseme nawe. Mwache akuambie kwamba alikuja kuijaza roho yako furaha tele. Na ujue kwamba kila anachokuletea unapewa kwa njia ya maombezi yenye utukufu ya Mama mkuu wa Mungu.

Bwana, nakushukuru kwa maisha tele ya neema unayonijalia. Nakushukuru kwa huu muujiza Wako wa kwanza, na kwa ujumbe unaonitumia mimi na wafuasi Wako wote. Nisaidie kuelekeza macho yangu Mbinguni na kwenye maisha ya furaha isiyo na kipimo yanayoningoja huko. Yesu, nakutumainia.


Neno Alifanyika Mwili

Jumapili ya Pili baada ya Noeli
(Wakati Sherehe ya Kutokewa kwa Bwana haihamishiwi Jumapili baada ya Januari 1)

Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kati yetu, nasi tukauona utukufu Wake, utukufu wa Mwana pekee wa Baba, aliyejaa neema na ukweli. Yohane 1:14

Kifungu hiki kutoka Injili ya Yohane kinatufunulia fumbo la Noeli. Neno wa milele wa Baba, Mwana wa Mungu, alitwaa mwili na kufanya makao Yake kati yetu. Uwepo Wake kati yetu unafunua utukufu wa Baba kwa kuwa Mwana pekee wa Baba “amejaa neema na ukweli.”

Ni rahisi kushindwa kuelewa maana kuu ya Krismasi. Ni rahisi kuiona kama simulizi zuri la tukio la zamani sana kuhusu kuzaliwa kwa mtoto, na kushindwa kuelewa fumbo kuu la Umwilisho.

Kwa kutwaa mwili wetu, Mungu anajiunganisha na hali yetu ya kibinadamu. Umwilisho Wake unajenga daraja kati ya Mungu na mwanadamu, ukiwawezesha wanadamu kuuona utukufu wa Mungu. Lakini kuuona utukufu wa Mungu kupitia fumbo la Umwilisho si jambo linalotokea kwa macho yetu ya mwili pekee. Ni lazima tulione fumbo kuu la Umwilisho kwa macho ya imani.

Kuliona fumbo la Umwilisho kwa macho ya imani kunamaanisha kwamba, kwa kweli, tunakutana na utukufu wa Mungu katika maisha yetu wenyewe. Kunamaanisha kwamba tunaigundua hadhi ya kuwa binadamu kwa kutambua ukweli huu wa ajabu: Mungu alifanyika mmoja wetu. Hili lapaswa kutujaza mshangao wenye kicho tunapofurahia jinsi Mungu alivyo karibu nasi.

Unapoendelea kusherehekea Krismasi, tafakari leo maneno haya rahisi: “Naye Neno alifanyika mwili.” Yatafakari kwa kina, yatazame kwa makini na usali ukiongozwa nayo. Ruhusu fumbo la Krismasi la Umwilisho wa Mungu lizame ndani zaidi na zaidi katika maisha yako.

Bwana, nakushukuru kwa Umwilisho Wako. Nakushukuru kwa shukrani za dhati kwa kufanyika mmoja wetu. Nisaidie kuuona utukufu Wako, kwa kuwa sasa upo katika asili ya kibinadamu, na nisaidie kuiona hadhi uliyotufunulia sisi sote kwa kutwaa mwili wetu wenyewe. Yesu, nakutumainia.


Kuabudu kwa Mamajusi

Kutokewa kwa Bwana
Januari 6, au Jumapili ya kwanza baada ya Januari 1

Walipoingia nyumbani walimwona mtoto pamoja na Maria mama Yake. Wakasujudu na kumheshimu. Kisha wakafungua hazina zao, wakamtolea zawadi za dhahabu, ubani na manemane. Mathayo 2:11

“Epifania” maana yake ni kujidhihirisha. Nayo “Epifania ya Bwana” ni kujidhihirisha kwa Yesu si kwa hawa Mamajusi watatu kutoka Mashariki tu, bali pia ni kujidhihirisha kwa Kristo kwa ulimwengu mzima, kwa njia ya ishara lakini kwa uhalisi. Mamajusi hawa, waliosafiri kutoka taifa la kigeni lisilo la Kiyahudi, wanadhihirisha kwamba Yesu alikuja kwa ajili ya watu wote na kwamba wote wanaitwa kumwabudu.

Mamajusi hawa walikuwa “watu wenye hekima” waliochunguza nyota na kuifahamu imani ya Wayahudi kwamba Masihi alikuwa anakuja. Yaelekea walikuwa na ujuzi wa sehemu kubwa ya hekima ya wakati huo, na imani ya Wayahudi kuhusu Masihi iliwavutia.

Mungu alitumia kitu walichokifahamu ili kuwaita wamwabudu Kristo.  Alitumia nyota.  Walifahamu nyota, na walipoiona nyota hii mpya na ya pekee juu ya Bethlehemu, walitambua kwamba jambo la pekee lilikuwa likitokea.  Kwa hiyo, fundisho la kwanza tunalopata hapa kwa maisha yetu wenyewe ni kwamba Mungu atatumia kile tunachokifahamu kutuita Kwake.  Itafute “nyota” ambayo Mungu anaitumia kukuita.  Iko karibu nawe kuliko unavyoweza kudhani.

Jambo la pili la kuzingatia ni kwamba Mamajusi walianguka kifudifudi mbele ya Mtoto Kristo.  Waliyaweka maisha yao mbele Yake kwa kujisalimisha kikamilifu na kumwabudu.  Walituwekea mfano mkamilifu.  Ikiwa wataalamu hawa wa nyota kutoka nchi ya kigeni waliweza kuja na kumwabudu Kristo kwa namna ya kina hivyo, nasi tunapaswa kufanya vivyo hivyo.  Pengine leo unaweza kujaribu kulala kifudifudi kweli unaposali, ukiwaiga Mamajusi, au angalau kufanya hivyo moyoni mwako kwa njia ya sala.  Mwabudu kwa kuyakabidhi maisha yako kikamilifu Kwake.

Mwisho, Mamajusi wanaleta dhahabu, ubani na manemane.  Zawadi hizi tatu, walizomtolea Bwana wetu, zinaonyesha kwamba walimtambua Mtoto huyu kuwa Mfalme wa Kimungu ambaye angekufa ili kutuokoa kutoka dhambini.  Dhahabu ni kwa ajili ya Mfalme, ubani ni sadaka inayoteketezwa kwa Mungu, na manemane hutumiwa kwa ajili ya mtu ambaye angekufa.  Hivyo, ibada yao inajengwa juu ya kweli kuhusu Mtoto huyu ni nani.  Ikiwa tunataka kumwabudu Kristo ipasavyo, lazima pia tumheshimu kwa namna hizi tatu.

Tafakari leo juu ya Mamajusi hawa, uwaone kama ishara ya kile unachoitwa kufanya.  Unaitwa kutoka katika mahali pa ugenini pa ulimwengu huu ili kumtafuta Masihi.  Mungu anatumia nini kukuita Kwake?  Unapomwona, usisite kukiri ukweli kamili kuhusu Yeye ni nani, ukilala kifudifudi mbele Yake kwa kujisalimisha kikamilifu na kwa unyenyekevu.

Bwana, ninakupenda na kukuabudu. Nayaweka maisha yangu mbele Yako na kukukabidhi yote. Wewe ndiwe Mfalme wangu wa Kimungu na Mwokozi wangu. Maisha yangu ni Yako. (Sali mara tatu kisha usujudu mbele ya Bwana) Yesu, nakutumainia.


Kuwatafuta Wenye Uhitaji

Siku ya Kwanza ya Juma ya Kipindi cha Noeli baada ya Kutokewa kwa Bwana
Jumatatu baada ya Kutokewa kwa Bwana (Au Januari 7)

Wakamletea Yesu wote waliokuwa na magonjwa mbalimbali na walioteswa na maumivu makali, waliopagawa na pepo, wenye kichaa na waliopooza, naye akawaponya. Mathayo 4:24b

Sasa kwa kuwa tumekamilisha maadhimisho yetu ya Oktava ya Noeli na pia tumeadhimisha Kutokea Bwana, tunaanza kuelekeza macho yetu kwenye huduma ya Yesu hadharani.  Injili ya leo inaonyesha mwanzo wa huduma Yake baada ya Yohane Mbatizaji kukamatwa.  Katika Injili hii, watu wengi waliokuwa na uhitaji waliletwa kwa Yesu.

Tunaweza kukiangalia kifungu hiki kwa mitazamo mbalimbali. Tunaweza kukiangalia kwa mtazamo wa huduma ya Yesu, kwa mtazamo wa wale walioponywa, lakini pia kwa mtazamo wa wale waliowaleta wengine kwa Yesu. Ni mtazamo huu wa mwisho tunaoutafakari leo.

Jiwazie ukiwa mmoja wa wale waliowaleta kwa Yesu watu wenye “maradhi mbalimbali,” wale “walioteswa na maumivu makali,” na wale “waliopagawa na pepo, wenye kichaa na waliopooza.”  Je, una upendo, kujali na huruma vinavyohitajika ili uwe mtu anayewaleta watu hawa kwa Yesu?

Mara nyingi, tunapokutana na wale wanaoteseka au “waliokataliwa” na jamii, tunaelekea kuwadharau.  Inahitaji mtu mwenye huruma na moyo wa kuwasikitikia sana wengine ili kuona hadhi ya watu hawa na kufanya jambo la kuwasaidia wapone na kukutana na upendo wa Mungu.  Kuwafikia wale walio katika uhitaji mkubwa kunahitaji unyenyekevu mkubwa kwa upande wetu na moyo ambao kwa kweli hauwahukumu wengine.  Mwana wa Mungu alikuja katika ulimwengu wetu kuwaletea watu wote uponyaji na wokovu.  Ni wajibu wetu kusaidia kuwaleta watu wote kwa Yesu, bila kujali hali yao, ukubwa wa uhitaji wao, au hadhi yao katika jamii.

Tafakari leo juu ya watu wa aina hii katika maisha yako mwenyewe.  Ni nani anayeteseka na mwenye uhitaji?  Ni nani ambaye unaweza kushawishika kumhukumu na kumkosoa?  Ni nani aliyevunjika moyo, mwenye huzuni, aliyechanganyikiwa, aliyepotoka au mgonjwa kiroho?  Pengine kuna watu wagonjwa kimwili ambao Mungu anakuita uwafikie, au pengine ni mtu mwenye ugonjwa wa akili, wa kimaadili au wa kiroho kwa namna fulani.  Unawatendeaje?  Injili ya leo inatuita tufuate mfano wa wanafunzi hawa wa kwanza wa Yesu kwa kuwatafuta wenye uhitaji na kutafuta njia za kuwaleta kwa Yesu, Mponyaji wa Kimungu.  Jitoe kutenda tendo hili la huruma, nawe utabarikiwa kwa wema wako.

Bwana, tafadhali nipe moyo wenye huruma na unaowasikitikia wengine.  Nisaidie kutambua kwamba ulikuja kwa ajili ya watu wote, hasa wale walio katika uhitaji mkubwa.  Nipe neema ya kutimiza wajibu wangu ili watu wote waje kuingia katika uwepo Wako unaoponya.  Yesu, nakutumainia.


Kumtumainia Yesu katika Mambo Yote

Siku ya Pili ya Juma katika Kipindi cha Noeli baada ya Epifania
Jumanne baada ya Epifania (Au Januari 8)

Wakati huo ilikuwa tayari jioni, na wanafunzi wa Yesu wakamkaribia na kusema, “Mahali hapa ni pa nyika, na muda umeenda sana. Waage watu waende kwenye mashamba na vijiji vya jirani wakajinunulie chakula.” Marko 6:35–36

Je, unamtumainia Yesu?  Tunahitaji kuwa na tumaini Kwake katika nyanja nyingi.  Tunahitaji kumtumainia ili kupokea nguvu zote za kiroho, kihisia na kisaikolojia tunazohitaji, si tu kuweza kuishi kila siku, bali pia kustawi kwa njia nyingi.  Tunahitaji pia kumtumainia Mungu kwamba atatutimizia mahitaji yetu ya msingi ya kila siku kama vile chakula, makazi na mavazi.  Kwa watu wengi, kumtumainia katika mambo haya si vigumu, lakini kwa wengine kunahitaji kujisalimisha kwa kiwango kikubwa sana.

Tukio hili la Injili linampa Yesu nafasi ya kupima tumaini la wanafunzi Wake Kwake. Mwanzoni, wanashindwa jaribu hilo kwa kuingiwa na hofu na kumwomba Yesu auage umati wa watu waende wakatafute chakula, lakini mwishowe wanajawa na mshangao wanapoona maongozi ya Mungu yakifanya kazi. Hatimaye, Yesu anaizidisha mikate mitano na samaki wawili ili kuwalisha watu zaidi ya elfu tano.

Kwanza kabisa, Injili hii haituambii kwamba tunaweza kupuuza wajibu wa kujipatia mahitaji yetu na kutumaini tu kwamba Yesu atatupatia kila kitu kwa muujiza kila wakati. Haimaanishi kuacha wajibu wetu wa kufanya kazi na kujipatia mahitaji yetu wenyewe na ya familia zetu.

Kiini cha Injili hii ni kumtumainia Mungu. Katika tukio hili, wafuasi wa Yesu walikuwa wakivutwa kumwelekezea Bwana wetu macho yao na kukaa Naye. Walikuwa wakivutwa kiroho kuacha mahangaiko yote ya maisha kwa wakati huo ili waweze kulishwa kiroho. Walikuwa wakialikwa kutenda tendo la imani, na ni wazi kwamba umati wa watu kwa kweli ulikuwa ukiuitikia kwa tumaini mwaliko huo wa ndani. Hilo linadhihirika kwa kuwa bado walikuwa pamoja Naye licha ya njaa yao ya kimwili iliyokuwa dhahiri.

Kwa hiyo, ujumbe mmoja muhimu ni kwamba wakati mwingine Mungu anatuita tumtumainie kwa namna ambazo hazionekani mara moja kuwa za kufaa au zenye mantiki. Jambo lililoonekana kufaa lingekuwa kuondoka na kujitafutia chakula. Lakini mwito wa neema upitao maumbile, wakati huo, uliambia kundi hili la watu elfu tano kwamba walipaswa kubaki pamoja na Yesu na kutumaini kwamba mambo yote yangekuwa sawa. Ndivyo walivyofanya, na mambo yakawa sawa.

Tafakari leo jinsi Mungu anavyokuita wakati mwingine umfuate kwa njia ambazo huzielewi mara moja. Usishangae ikiwa nyakati fulani unahisi Mungu akikuita usikilize kwa makini zaidi ahadi Yake ya kukutunza kuliko hitimisho unalofikia kwa kufuata mantiki ya kibinadamu tu. Njia za Mungu ziko juu sana kuliko njia zetu. Wakati mwingine wito Wake unadai mabadiliko makubwa, na unapokuwa na hakika ya ndani kabisa katika imani kwamba Mungu anakuita umtumainie, basi fanya hivyo. Mtumainie katika mambo yote, naye atakutimizia mahitaji yako daima.

Bwana, tumaini langu Kwako wakati mwingine ni dhaifu. Wakati mwingine ninautilia shaka wema Wako na maongozi Yako katika maisha yangu. Nisaidie daima kuutumainia mwaliko Wako wa upole kuliko mahitimisho yangu mwenyewe maishani. Nisaidie kuongozwa Nawe daima ili niishi kila siku kulingana na mpango Wako mkamilifu. Yesu, nakutumainia.


Kutafakari Uzoefu wa Neema

Siku ya Tatu ya Juma katika Kipindi cha Noeli baada ya Epifania
Jumatano baada ya Epifania (Au Januari 9)

Baada ya wale elfu tano kula na kushiba, Yesu aliwaamuru wanafunzi Wake wapande mashua na kumtangulia kwenda ng’ambo kuelekea Bethsaida, huku Yeye akiwaaga watu. Naye alipokwisha kuwaaga, alikwenda mlimani kusali. Marko 6:45–46

Watu walikuwa wanafikiria nini Yesu alipowaacha? Walikuwa wamekaa naye kwa siku kadhaa bila chakula, Yesu akaizidisha mikate mitano na samaki wawili ili kuwalisha wote, wakastaajabia kulishwa huko kwa muujiza, kisha Yesu akawaacha na kwenda peke Yake kusali. Wazia mawazo yao na mazungumzo ambayo watu hao wangekuwa nayo kutokana na tukio hili!

Huenda baadhi yao wangejaribu kutafuta maelezo ya kimantiki kuhusu kuongezeka kwa chakula, wengine wangeamini kwa moyo wote kwamba ulikuwa muujiza, na wengine wasingekuwa na hakika wafikiri nini. Hali hii ndiyo tunayoipitia mara nyingi tunapokutana na nguvu na neema ya Mungu katika maisha yetu.

Huenda tusione miujiza halisi ya kimwili kila siku. Kwa kweli, huenda tusishuhudie hata mmoja katika maisha haya. Lakini tukiwa wazi kumpokea Mungu, tutatambua mara kwa mara nguvu Yake iliyo hai katika maisha yetu. Mara nyingi itajidhihirisha kwa namna ya hila na iliyofichika, lakini nyakati fulani itakuwa wazi na kuleta mabadiliko. Swali la kwanza ni ikiwa tuna macho ya imani ya kuona Mungu akitenda kazi, na swali la pili ni ikiwa tunaruhusu matendo Yake yatubadilishe.

Makundi ya watu yalipokuwa yakitawanyika, Mungu angekuwa akiwauliza swali hili la pili ndani ya mioyo yao. Walikuwa wametoka tu kushuhudia nguvu za Mungu, na sasa, baada ya kupitia tukio hili, kila mmoja wao aliitwa kuliruhusu limbadilishe. Waliitwa waondoke huku wakilitafakari kwa furaha lililotokea, wakiliamini na kuliruhusu liingie ndani kabisa ya mioyo yao.

Tafakari leo juu ya uwepo wa Mungu katika maisha yako. Mungu amezungumza nawe kwa namna gani, amekusaidiaje na amekuwa nawe vipi ulipokuwa na uhitaji? Ni rahisi kusahau upesi yale anayofanya Mungu. Lengo ni kuyatunza moyoni yote aliyotenda na kuruhusu matendo hayo yaendelee kuitunza mioyo yetu. Leo, tafakari matendo Yake ya wakati uliopita ili matendo hayo ya upendo wa Mungu yaendelee kuzaa matunda katika maisha yako leo.

Bwana, ninajua kwamba umekuwa hai na ukitenda kazi katika maisha yangu kwa namna zisizohesabika. Nisaidie kuzihifadhi daima zawadi hizo za neema. Nisaidie kuruhusu uwepo Wako katika maisha yangu uwe chemchemi ya daima ya kuutumainia mpango Wako mkamilifu. Na inapoonekana kana kwamba umeondoka, nisaidie kujua kwamba Wewe uko karibu daima na unatenda kazi daima katika maisha yangu. Yesu, nakutumainia.


Jukumu la Kinabii la Kristo

Siku ya Nne ya Juma katika Kipindi cha Noeli baada ya Epifania
Alhamisi baada ya Epifania (Au Januari 10)

Yesu akawaambia, “Leo kifungu hiki cha Maandiko kimetimia mkiwa mnasikia.” Wote wakamsifu na kustaajabia maneno yenye neema yaliyotoka kinywani Mwake. Luka 4:21–22a

Yesu alikuwa amewasili Nazareti, alikokulia, akaingia katika eneo la Hekalu kusoma Maandiko. Alisoma kifungu kutoka kwa Isaya: “Roho wa Bwana yu juu yangu, kwa sababu amenipaka mafuta niwaletee maskini habari njema. Amenituma niwatangazie mateka uhuru na vipofu kupata kuona tena, niwaache huru wanaodhulumiwa, na kutangaza mwaka unaokubalika kwa Bwana.” Baada ya kusoma hayo, aliketi na kutangaza kwamba unabii huo wa Isaya ulikuwa umetimia.

Mwitikio wa watu wa mji Wake unavutia. Wao “wote walimsifu na kustaajabia maneno ya neema yaliyotoka kinywani Mwake.” Angalau, huo ndio ulikuwa mwitikio wao wa kwanza. Lakini tukiendelea kusoma, tunaona kwamba Yesu anawapa watu hao changamoto na, kwa sababu hiyo, walijawa na hasira kali na kujaribu kumuua papo hapo.

Mara nyingi, sisi huitikia kwa namna hiyo hiyo kwa Yesu. Mwanzoni, tunaweza kumsifu na kumpokea kwa moyo mkunjufu. Kwa mfano, wakati wa Krismasi tunaweza kuimba nyimbo za Krismasi na kusherehekea siku Yake ya kuzaliwa kwa furaha na shangwe. Tunaweza kwenda kanisani na kuwatakia watu Krismasi njema. Tunaweza kuandaa pango la Krismasi na kupamba kwa alama za Kikristo za imani yetu. Lakini haya yote yana kina gani? Wakati mwingine sherehe na desturi za Krismasi ni za juu juu tu na hazionyeshi kina chochote cha kweli cha msimamo au imani ya Kikristo. Nini hutokea wakati Mtoto huyu mpendwa, Kristo, anaposema maneno ya ukweli na usadikisho? Nini hutokea wakati Injili inapotuita tutubu na kuongoka? Tunamwitikiaje Kristo katika nyakati hizo?

Tunapoendelea na juma la mwisho la kipindi chetu cha Krismasi, tafakari leo ukweli kwamba Mtoto mdogo tunayemheshimu wakati wa Krismasi amekua na sasa anatuambia maneno ya ukweli. Tafakari kama uko tayari kumheshimu si tu kama mtoto mchanga, bali pia kama Nabii wa Ukweli wote. Je, uko tayari kusikiliza ujumbe Wake wote na kumpokea kwa furaha? Je, uko tayari kuruhusu maneno Yake ya Ukweli yapenye moyoni mwako na kuyageuza maisha yako?

Bwana, ninakupenda na ninatamani kwamba yote uliyosema yapenye moyoni mwangu na kuniongoza katika ukweli wote. Nisaidie nikukubali si tu kama mtoto mdogo aliyezaliwa Bethlehemu, bali pia kama Nabii mkuu wa Ukweli. Nisije kamwe nikachukizwa na maneno unayosema, na niwe daima tayari kupokea kazi Yako ya kinabii katika maisha yangu. Yesu, nakutumainia.


Kusujudu Mbele ya Yesu

Siku ya Tano ya Juma katika Kipindi cha Noeli baada ya Epifania
Ijumaa baada ya Epifania (Au Januari 11)

Ikawa kwamba katika mojawapo ya miji ambamo Yesu alikuwamo, kulikuwa na mtu aliyejaa ukoma. Alipomwona Yesu, akasujudu, akamsihi akisema, “Bwana, ukitaka, unaweza kunitakasa.” Yesu akanyosha mkono Wake, akamgusa na kusema, “Nataka. Takasika.” Luka 5:12–13a

Kwa mara nyingine tena, tunaona taswira ya kusujudu mbele ya Bwana wetu. Wakati huu anayesujudu ni mwenye ukoma. Lakini juma hili lililopita tu, tulipoadhimisha Kutokea kwa Bwana, tulikumbushwa kuhusu Mamajusi watatu kutoka Mashariki ambao pia walikuja kumwabudu Kristo na kusujudu mbele Yake.

Labda sisi sote tungependa kujiona kama Mamajusi, tukija kumtafuta Kristo tukiwa watu wenye hadhi na wanaovutiwa na wengine katika jamii. Bila shaka Mamajusi wangeonekana hivyo. Hata hivyo, hatupaswi kukosa pia kujiona kuwa tunafanana na huyu mwenye ukoma aliyemjia Yesu katika udhaifu na unyonge wake, akisujudu mbele ya Bwana wetu na kuomba huruma. Hapana, huenda hatuna ukoma kwa maana halisi, lakini sisi sote tunamjia Yesu tukiwa wagonjwa na wenye kuhitaji huruma Yake na mguso Wake wa uponyaji.

Angalia alichofanya Yesu. “Alinyosha mkono Wake, akamgusa,” kisha akamponya. Yesu hakusita, hakumtendea mwenye ukoma kwa dharau yoyote, wala hakukosa huruma hata kidogo. Mara moja Yesu alimimina neema Yake ya uponyaji katika maisha ya mwenye ukoma.

Tunapokaribia mwisho wa kipindi cha Krismasi pamoja na adhimisho lijalo la Ubatizo wa Bwana, tunapaswa kukumbuka kwamba sisi sote tumeguswa na Kristo katika Ubatizo. “Mguso” huu unaendelea katika maisha yetu yote. Ni mguso unaotutakasa na kutugeuza. Ni mguso unaoponya na kufariji. Jiruhusu kuonja huruma ya Yesu kwa kumjia kwa unyenyekevu huku ukitambua hitaji lako la neema. Usiogope kujikabidhi Kwake kabisa, ukijua kwa hakika kwamba hatasita hata kwa muda mfupi kukufikia na kukujalia wingi wa huruma Yake.

Bwana, ukitaka, waweza kunitakasa. Ukitaka, waweza kuniponya, kunisamehe, kuniimarisha na kunipenda. Ninakushukuru mapema kwa sababu ninajua kwamba unatamani na unachagua kunibariki kwa njia hizi na kwa kila njia nyingine ninayohitaji. Asante kwa huruma na neema Yako, na asante kwa kunikubali katika udhaifu wangu. Ninakupenda, Bwana wangu, nami nachagua kusujudu mbele Yako kwa upendo na ibada. Yesu, nakutumainia.


Kanuni Inayoongoza Maisha Yako

Siku ya Sita ya Juma katika Kipindi cha Noeli baada ya Epifania
Jumamosi baada ya Epifania (Au Januari 12)

“Yeye hana budi kuongezeka; mimi nina budi kupungua.” Yohane 3:30

Maneno haya yenye nguvu na ya kinabii ya Mtakatifu Yohane Mbatizaji yanapaswa kusikika mioyoni mwetu kila siku. Yanasaidia kuipa mwelekeo hali yetu yote ya sasa na namna tunavyopaswa kuwa. Maneno haya yanamaanisha nini? Ni wazi kwamba kuna mambo mawili ambayo Yohane anasema hapa: 1) Yesu hana budi kuzidi, 2) Sisi hatuna budi kupungua.

Kwanza kabisa, Yesu kuzidi katika maisha yetu ndilo lengo kuu tunalopaswa kuwa nalo. Hili linamaanisha nini hasa? Linamaanisha kwamba anazidi kutawala akili na utashi wetu. Linamaanisha kwamba sisi ni Wake, naye ni wetu. Linamaanisha kwamba lengo letu la kwanza na shauku yetu kuu maishani ni kutimiza mapenzi Yake matakatifu katika mambo yote. Linamaanisha kwamba hofu inawekwa kando na mapendo yanakuwa sababu yetu ya kuishi. Kumruhusu Bwana azidi katika maisha yetu hutuweka huru sana. Hutuweka huru kwa maana kwamba hatuhitaji tena kujaribu kuyamudu maisha kwa nguvu zetu wenyewe. Sasa Yesu anaishi ndani yetu na kwa njia yetu.

Pili, Yohane anaposema kwamba yeye lazima apungue, anamaanisha kwamba utashi wake mwenyewe, matamanio, malengo, matumaini yake, na mengineyo, lazima viyeyuke kadiri Yesu anavyoshika hatamu. Inamaanisha kwamba ubinafsi wote lazima uachwe, na kuishi bila ubinafsi lazima kuwe kanuni ya msingi ya maisha yetu. “Kupungua” mbele ya Mungu kunamaanisha kuwa wanyenyekevu. Unyenyekevu ni njia ya kuacha kila kitu kisichotokana na Mungu na kumruhusu Mungu pekee aangaze kupitia sisi.

Tafakari leo kauli hii nzuri ya Mtakatifu Yohane Mbatizaji. Ifanye kuwa sala na uirudie tena na tena. Iache iwe kanuni inayoongoza maisha yako.

Bwana, Wewe lazima uzidi, nami lazima nipungue. Tafadhali njoo uitawale kabisa roho yangu. Badilisha akili na moyo wangu, ongoza utashi, hisia na matamanio yangu. Unijalie kuwa chombo kitakatifu cha uzima Wako wa kimungu. Yesu, nakutumainia.


“Nimependezwa Nawe Sana”

Ubatizo wa Bwana
Jumapili baada ya Januari 6

Baada ya watu wote kubatizwa, na Yesu pia kuwa amebatizwa, alipokuwa akisali, mbingu ilifunguka na Roho Mtakatifu akashuka juu Yake kwa umbo la mwili kama njiwa. Sauti ikatoka mbinguni, “Wewe ndiwe Mwanangu mpendwa; nimependezwa nawe sana.” Luka 3:21–22 (Injili ya Mwaka C)

Sikukuu ya leo inaadhimisha mwisho wa Kipindi cha Noeli na mwanzo wa Kipindi cha Kawaida. Ni sikukuu ya mpito kutoka maisha ya Yesu yaliyofichika hadi huduma Yake ya hadharani. Pia inarudia ujumbe wa Epifania, kwa kuwa Ubatizo wa Bwana ni udhihirisho mwingine unaotangaza umungu wa Yesu kwa wafuasi Wake wote wa kwanza na kwa wanafunzi wa Yohane Mbatizaji.

Kwanza kabisa, inapaswa kuelezwa wazi kwamba Yesu hakuhitaji ubatizo wa Yohane. Yohane alikuwa akibatiza kama mwito wa toba ya ndani na ishara yake. Yesu hakuwa na haja ya kutubu. Lakini, hata hivyo, anamwendea Yohane. Mwanzoni Yohane anakataa, lakini Yesu anasisitiza. Kwa nini alipokea ubatizo?

Kwanza, kwa kuukubali ubatizo wa Yohane, Yesu anathibitisha yote ambayo Yohane amesema na kufanya, na anathibitisha jukumu lake takatifu la kumwandalia Yesu njia na kuandaa kipindi kipya cha neema.  Kwa hiyo, Ubatizo wa Yesu unakuwa daraja kati ya manabii wa Agano la Kale (ambao Yohane alikuwa wa mwisho wao) na kipindi cha Agano Jipya cha neema na ukweli.

Pili, imesemwa kwamba Yesu alipoingia katika maji ya ubatizo, hakubatizwa na maji hayo; bali, Ubatizo Wake ulikuwa ule ambao ndani yake maji yote yaliyoumbwa katika ulimwengu huu, kwa namna fulani, “yalibatizwa” Naye.  Kwa kuingia katika maji, Yesu aliyatakatifuza maji na kuimimina neema Yake, akiyafanya maji yote kuwa chanzo cha wokovu kwa wakati ujao.

Tatu, Ubatizo wa Yesu ulikuwa epifania.  Ulikuwa wakati wa udhihirisho.  Alipopanda kutoka majini, “Mbingu zilifunguka na Roho Mtakatifu akashuka juu Yake kwa umbo la mwili kama njiwa.  Na sauti ikatoka Mbinguni, ‘Wewe ni Mwanangu mpendwa; nimependezwa Nawe.’”  Udhihirisho huu wa Yesu kuwa Mwana na wa umungu Wake ulitokea kwa namna ya kimwili, inayosikika na kuonekana, ili wote waliokuwapo wajue bila shaka kwamba Yesu alikuwa Mwana wa Baba.  Hivyo, ubatizo Wake ulikuwa namna ambayo Baba alimtambulisha Mwanawe na utume wa Mwanawe kwa ulimwengu.

Tunapojiandaa kuanza Kipindi cha Mwaka, tafakari leo maneno haya ya Baba wakati wa Ubatizo wa Yesu. Msikilize Baba akikuambia kuhusu umungu wa Mwanawe. Mwelekezee Yesu macho yako na ujiandae kumfuata na kulisikiliza kwa makini kila neno analosema. Alitumwa ulimwenguni humu ili atuvute kwa Baba; mruhusu autimize utume huo katika maisha yako mwenyewe.

Bwana, ninaamini kwamba Wewe ni Mwana wa Baba wa Milele na Mwokozi wa Ulimwengu. Ninaamini kwamba umeleta enzi mpya ya neema na ukweli, na kwamba nimeitwa kukufuata popote unaponiongoza. Tunapoanza kipindi hiki cha kiliturujia cha Kipindi cha Mwaka, na kiwe wakati wa neema ya pekee ambamo kila siku ninaisikiliza kwa makini sauti Yako. Yesu, nakutumainia.

 

Sikukuu na Sherehe

Yaliyomo


Pia Kinapatikana kama Kitabu chenye Jalada Laini & Kitabu cha Kielektroniki

Amazon.com – Google Play – iTunes – Barnes and Noble

Shiriki ukurasa huu: