Kiswahili

Juma la Thelathini la Kipindi cha Kawaida

Amri Kuu Kuliko Zote

Jumapili ya Thelathini ya Kipindi cha Kawaida (Mwaka A)

“Mwalimu, ni amri ipi katika sheria iliyo kuu kuliko zote?”  Mathayo 22:36

Swali hili liliulizwa na mmoja wa wataalamu wa sheria kwa nia ya kumjaribu Yesu.  Kutokana na muktadha wa kifungu hiki, ni wazi kwamba uhusiano kati ya Yesu na viongozi wa dini wa wakati Wake ulikuwa unaanza kuwa wa mabishano.  Walikuwa wanaanza kumjaribu na hata kutafuta kumtega. Hata hivyo, Yesu aliendelea kuwanyamazisha kwa maneno Yake ya hekima.

Akijibu swali hilo, Yesu anamnyamazisha mtaalamu huyu wa sheria kwa kutoa jibu kamilifu.  Anasema, “Utampenda Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, na kwa akili yako yote.  Hii ndiyo amri kuu kuliko zote na ya kwanza.  Ya pili inafanana nayo: Utampenda jirani yako kama nafsi yako” (Mathayo 22:37-39).

Kwa kauli hii, Yesu anatoa muhtasari kamili wa sheria ya maadili iliyo katika Amri Kumi. Amri tatu za kwanza zinafunua kwamba tunapaswa kumpenda Mungu kuliko yote na kwa nguvu zetu zote. Amri saba za mwisho zinafunua kwamba tunapaswa kumpenda jirani yetu. Sheria ya maadili ya Mungu ni rahisi: kuzitimiza amri hizi mbili zinazojumuisha zile nyingine zote.

Lakini je, yote hayo ni rahisi kiasi hicho?  Kwa kweli, jibu ni “Ndiyo” na pia “Hapana.”  Ni rahisi kwa maana kwamba kwa kawaida mapenzi ya Mungu si jambo lenye utata na gumu kuelewa.  Upendo umeelezwa wazi katika Injili, nasi tunaitwa kukubali kuishi maisha ya upendo wa kweli na mapendo yanayohusisha nafsi yetu nzima.

Hata hivyo, inaweza kuonekana kuwa ngumu kwa sababu hatuitwi kupenda tu, bali tunaitwa kupenda kwa utu wetu wote. Tunapaswa kujitoa kikamilifu na bila kujibakizia chochote. Hili linadai kujitoa kwa dhati kabisa, bila kuzuia chochote.

Tafakari leo juu ya wito huu rahisi wa kumpenda Mungu na jirani yako kwa utu wako wote. Tafakari hasa neno hilo “wote.” Unapofanya hivyo, bila shaka utatambua namna unavyoshindwa kujitoa kikamilifu. Unapoona kushindwa kwako, jitoe tena kwa matumaini kuifuata njia tukufu ya kujitoa kikamilifu kwa Mungu na kwa wengine.

Bwana wangu mwenye upendo, ninachagua kukupenda kwa moyo wangu wote, akili yangu yote, roho yangu yote na nguvu zangu zote. Pia ninachagua kuwapenda watu wote kama Wewe unavyowapenda. Nipe neema ya kuziishi amri hizi mbili za upendo na kuziona kama njia ya kuishi maisha matakatifu. Ninakupenda kweli, Bwana mpendwa. Nisaidie nikupende zaidi. Yesu, nakutumainia.


Yesu, Uwe na Huruma!

Jumapili ya Thelathini ya Kipindi cha Kawaida (Mwaka B)

Aliposikia kwamba alikuwa Yesu wa Nazareti, Bartimayo alianza kupaza sauti akisema, “Yesu, mwana wa Daudi, nihurumie.” Marko 10:47

Maneno haya ya Bartimayo, yule kipofu, yanatupatia sala kamilifu kwa sababu kadhaa.

Kwanza, sala hii inaonyesha unyenyekevu mkubwa wa Bartimayo.  Kwa kusali sala hii, Bartimayo anaonyesha kwamba alijua kuwa Yesu ndiye chanzo cha kile alichohitaji na kwamba hakuweza kujisaidia mwenyewe.  Bartimayo alijua kwamba alikuwa dhaifu lakini Yesu alikuwa nguvu kamilifu.  Kwa hiyo, katika uhitaji wake, alimgeukia Yesu kwa unyenyekevu, akimtambua kuwa ndiye chanzo.

Pili, ni sala inayolia kuomba “huruma.”  Huruma ni hisia ya huzuni na sikitiko inayosababishwa na mateso ya wengine.  Huruma ni rehema na ni namna ya upendo anayopewa mtu na mwingine ambaye hana ulazima wa kuutoa.  Katika sala hii, Bartimayo anamwomba Bwana mwenyezi amwonyeshe wema na huruma ingawa hastahili zawadi kama hiyo.  Sala hii inaonyesha kwamba Bartimayo alijua kuwa hakustahili msaada kutoka kwa Bwana wetu, lakini hata hivyo aliulilia kwa matumaini kwamba Yesu angemsaidia.  Na kwa kweli, Yesu anamsaidia.

Tatu, sala hii inafunua ari ya pekee na ya kina. Si ombi tu la kuomba msaada wa Mungu, bali ni kilio cha kuomba msaada. Ni kusihi na namna ya kuomba kwa unyenyekevu mkubwa. Ni kuifungua roho yako kwa Mungu, bila kuhofia kuonyesha udhaifu wako mwenyewe, wala kuwa na wasiwasi kwamba wengine wataona au watafikiria nini. Hili linaonyesha kina cha sala ya yule kipofu.

Tafakari leo juu ya mafundisho haya matatu kutoka katika sala fupi ya Bartimayo. Tunapaswa kuwa wanyenyekevu, kuomba huruma kwa kusihi, na kufanya hivyo kwa ari na shauku kubwa. Kusali hivi bila shaka kutatuandaa kuipokea neema na huruma ya Mungu.

Bwana Yesu, Mwana wa Daudi, nihurumie. Ninakusihi kwa unyenyekevu kwa moyo wangu wote unijalie huruma na rehema Zako. Ingawa sistahili, ninaitafuta neema Yako na kuutumainia wema Wako. Yesu, nakutumainia.


Haki ya Kweli

Jumapili ya Thelathini ya Kipindi cha Kawaida (Mwaka C)

Yesu aliwaambia mfano huu wale waliokuwa na hakika kwamba wao ni wenye haki na waliowadharau wengine wote.   Luka 18:9

Kifungu hiki cha Maandiko ni utangulizi wa Mfano wa Mfarisayo na Mtoza Ushuru.  Mfano huu unaonyesha tofauti kubwa kati ya mitazamo miwili ya jumla.  Kwanza, mtazamo wa Mfarisayo unaonyesha kwamba anajivunia sana nafsi yake, anaipa umuhimu mkubwa sifa yake mbele ya watu, na hatambui dhambi yake mwenyewe.  Pili, mtazamo wa mtoza ushuru unaonyesha kwamba anatambua kwa kina dhambi yake mwenyewe, anaisikitikia na anajua kuwa anahitaji huruma ya Mungu.  Matokeo ya mitazamo hii miwili tofauti sana ni kwamba mtoza ushuru alirudi nyumbani akiwa amehesabiwa haki, lakini Mfarisayo hakuhesabiwa haki.

Kuhesabiwa haki kunamaanisha nini? Kunamaanisha kwamba mtoza ushuru alikuwa na dhamiri safi na alisimama katika ukweli. Alijua kwamba alihitaji huruma, akaiomba kwa unyenyekevu na akaipokea. Hakujidanganya mwenyewe, wala kuwadanganya wengine au Mungu. Alijua yeye ni nani, na ukweli huo ndio uliomruhusu Mungu kumwinua. Mtoza ushuru alihesabiwa haki kwa kusamehewa dhambi zake na kujaliwa huruma ya Mungu katika maisha yake.

Huenda yule Farisayo alijisikia vizuri kwa kiasi fulani kwa sababu alijiinua ili wote wamwone. Alikuwa na hakika ya uadilifu wake mwenyewe, lakini kwa kweli hakuwa mwenye haki. Alikuwa akijiona tu kuwa mwenye haki machoni pake mwenyewe. Alikuwa akiishi katika uongo, na kuna uwezekano mkubwa kwamba aliuamini uongo huo, na huenda hata alikuwa amewashawishi wengine wauamini. Lakini ukweli ulibaki kuwa yule Farisayo hakuwa mwenye haki, wala hakuwa amehesabiwa haki kwa kweli.

Tunachopaswa kujifunza kutokana na kifungu hiki ni kutambua kwa kina umuhimu wa kuishi katika ukweli. Wale wanaojionyesha kuwa watu ambao si wao wanaweza kujidanganya na hata kuwadanganya wengine. Lakini hawatamdanganya Mungu kamwe, wala hawataweza kupata amani ya kweli rohoni mwao. Kila mmoja wetu anapaswa kutambua kwa unyenyekevu ukweli wa dhambi na udhaifu wake, na kwa utambuzi huo, kuisihi dawa pekee iliyopo—huruma ya Mungu.

Tafakari leo juu ya sala ya mtoza ushuru huyu: “Ee Mungu, unihurumie mimi mwenye dhambi” (Luka 18:13). Ifanye iwe sala yako. Kiri dhambi yako. Tambua kwamba unahitaji huruma ya Mungu na uiruhusu huruma hiyo ikuinue katika haki ya Mungu.

Bwana wa haki yote, Yesu Kristo, tafadhali unihurumie, kwa maana mimi ni mwenye dhambi. Ninakiri dhambi yangu na udhaifu wangu, nami ninaisihi huruma Yako tele. Tafadhali nimiminie huruma Yako na unisaidie kuufungua moyo wangu kwa yote unayotaka kunijalia. Nisaidie kuishi kwa unyenyekevu katika ukweli, Bwana mpendwa. Yesu, nakutumainia.


Yesu Anaponya

Jumatatu ya Wiki ya Thelathini ya Kipindi cha Kawaida

Yesu alikuwa akifundisha katika sinagogi siku ya Sabato. Na hapo alikuwapo mwanamke ambaye kwa miaka kumi na minane alikuwa amelemazwa na pepo; alikuwa amepinda mgongo, asiweze kabisa kusimama wima. Yesu alipomwona, alimwita na kumwambia, “Mwanamke, umewekwa huru kutokana na udhaifu wako.” Akaweka mikono Yake juu yake, naye mara moja akasimama wima na kumtukuza Mungu. Luka 13:10-13

Kila muujiza wa Yesu kwa hakika ni tendo la upendo kwa mtu anayeponywa. Katika simulizi hili, mwanamke huyu alikuwa ameteseka kwa miaka kumi na minane, na Yesu anamwonyesha huruma kwa kumponya. Na ingawa hilo ni tendo la wazi la upendo kwake yeye mwenyewe, simulizi hili lina mengi zaidi ya kutufundisha.

Ujumbe mmoja tunaoweza kupata katika simulizi hili unatokana na ukweli kwamba Yesu anaponya kwa hiari Yake mwenyewe. Ingawa baadhi ya miujiza hufanywa kwa ombi na sala ya yule anayeponywa, muujiza huu unatokana tu na wema wa Yesu na huruma Yake. Inaonekana mwanamke huyu hakuwa akitafuta uponyaji, lakini Yesu alipomwona, alimwonea huruma moyoni Mwake na akamponya.

Ndivyo ilivyo kwetu pia: Yesu anajua tunachohitaji kabla hatujamwomba. Wajibu wetu ni kubaki waaminifu Kwake daima na kujua kwamba, tunapokuwa waaminifu, atatupa tunachohitaji hata kabla hatujaomba.

Ujumbe wa pili unatokana na ukweli kwamba mwanamke huyu “alisimama wima” mara tu alipoponywa. Hii ni picha ya mfano ya kile ambacho neema hufanya ndani yetu. Mungu anapoingia katika maisha yetu, tunaweza kusimama wima, kwa kusema kwa mfano. Tunaweza kutembea tukiwa na ujasiri mpya na hadhi. Tunatambua sisi ni nani na kuishi kwa uhuru katika neema Yake.

Tafakari leo juu ya mambo haya mawili ya kweli. Mungu anajua kila hitaji ulilo nalo, naye atayatimiza mahitaji hayo wakati utakaokuwa bora zaidi kwako. Pia, anapokujalia neema Yake, itakuwezesha kuishi kwa kujiamini kikamilifu kama mwana Wake wa kiume au wa kike.

Bwana wa neema yote, ninajikabidhi Kwako na kuitumainia huruma Yako tele. Ninatumaini kwamba utaniwezesha kuenenda katika njia Zako kila siku ya maisha yangu kwa kujiamini kikamilifu. Yesu, nakutumainia.


Kuongoka kwa Moyo

Jumanne ya Wiki ya Thelathini ya Kipindi cha Kawaida

Akasema tena, “Nitaufananisha Ufalme wa Mungu na nini? Ni kama chachu ambayo mwanamke aliichukua na kuichanganya katika vipimo vitatu vya unga wa ngano mpaka donge lote likachachuka.” Luka 13:20-21

Chachu ni kitu cha kuvutia sana. Ni ndogo sana, lakini ina athari kubwa ajabu katika donge la unga. Chachu hufanya kazi polepole na kwa namna inayofanana na muujiza. Kidogo kidogo donge la unga hufura na kubadilika. Daima watoto huvutiwa kutazama jambo hili wakati wa kutengeneza mkate.

Hii ndiyo namna bora ya Injili kufanya kazi katika maisha yetu. Sasa hivi, Ufalme wa Mungu uko hai kwanza kabisa katika mioyo yetu. Ni mara chache sana kuongoka kwa mioyo yetu hutokea kwa ufanisi katika siku moja au kwa muda mfupi tu. Bila shaka, kila siku na kila wakati ni muhimu, na kwa hakika kuna nyakati zenye nguvu za kuongoka ambazo sote tunaweza kuzitaja. Lakini kuongoka kwa moyo kunafanana zaidi na chachu inayofanya donge la unga liumuke. Kwa kawaida, kuongoka kwa moyo ni jambo linalotokea kidogo kidogo na hatua kwa hatua. Tunamruhusu Roho Mtakatifu ayaongoze maisha yetu kwa undani unaozidi kuongezeka na, tunapofanya hivyo, tunazidi kukua katika utakatifu, kama vile donge linavyoumu​ka polepole lakini kwa hakika.

Tafakari leo juu ya mfano huu wa chachu inayofanya donge la unga liumuke.  Je, unaona huu kuwa mfano wa nafsi yako?  Je, unamwona Roho Mtakatifu akifanya kazi ndani yako kidogo kidogo?  Je, unaona ukibadilika polepole lakini bila kukoma?  Tunatumaini kwamba jibu ni “Ndiyo.”  Ingawa kuongoka huenda kusitokee sikuzote mara moja, ni lazima kuendelee daima ili kuiwezesha nafsi kusonga mbele kuelekea mahali pale ilipoandaliwa na Mungu.

Bwana, ninatamani kweli kuwa mtakatifu. Ninatamani kubadilishwa kidogo kidogo kila siku. Nisaidie nikuruhusu unibadilishe kila wakati wa maisha yangu ili niweze kuendelea kutembea katika njia uliyoniwekea. Yesu, nakutumainia.


Kujiamini Kupita Kiasi

Jumatano ya Wiki ya Thelathini ya Kipindi cha Kawaida

“Ndipo atawaambia, ‘Sijui mnakotoka.  Ondokeni kwangu, ninyi nyote mtendao maovu!’”  Luka 13:27

Yesu anaweka wazi kwamba kuna baadhi ya watu watakaokuja Kwake wakijichukulia kuwa hakika wataingia Mbinguni, lakini dhana yao hiyo itakabiliwa na maneno haya ya kutisha: “Sijui mnatoka wapi. Ondokeni kwangu.”

Kujiamini kupita kiasi ni dhambi hatari.  Ni hatari kwa sababu mbili.  Kwanza, watu wanapojiamini kupita kiasi, wanaishi huku wakiukana ukweli.  Kuhusu Mungu, kujiamini kupita kiasi kunamaanisha kwamba watu wanatenda kana kwamba wana uhusiano na Mungu ilhali hawana.  Wanaweza kusema mambo matakatifu, kutenda kwa namna inayoonekana kuwa takatifu na hata kuamini kwamba wao ni watakatifu, wakati kwa kweli hawamjui Bwana wetu hata kidogo.  Hivyo, kujiamini kupita kiasi ni hali ya mtu kuishi huku akiukana ukweli.

Pili, kujiamini kupita kiasi ni hatari kwa sababu mtu anayejiamini hivyo hatatubu dhambi yake mwenyewe. Hii ni kwa sababu kuukana ukweli kunamfanya ashindwe kukiri dhambi yake.  Bila kukiri dhambi yake, hawezi kisha kukiri kwamba anahitaji kubadilika.  Anabaki amezama katika mawazo yake potovu na dhambi yake.

Yesu anatoa fundisho hili si ili kuonyesha kwamba Yeye ni mkali kwa wale wanaojitumainia kupita kiasi; bali analitoa kama tendo la huruma kubwa kwa wale waliokwama katika dhambi hii.  Ufunuo huu wa kushtua unahitajika ili kumzindua mtu na kumweka huru kutoka katika dhambi hii.  Katika hali hii, ni hofu ya siku moja kusikia maneno haya kutoka kwa Yesu itakayowasaidia wale waliokwama katika kujitumainia kupita kiasi kujinasua na kuukabili ukweli.

Tafakari leo juu ya namna yoyote ambayo husemi ukweli kwako mwenyewe au kwa wengine.  Acha mshtuko wa kujua matokeo ya mwisho ya kujiamini kokote kupita kiasi katika maisha yako ukuzindue na kukuweka huru kutoka katika dhambi hii, ili uweze kujinyenyekeza mbele za Mungu sasa, kabla hujachelewa mno.  Kumbuka jinsi Bwana wetu anavyokupenda kwa dhati, na uuache upendo huo ukusaidie kuyakabili maisha yako kwa ukweli na uadilifu.

Bwana wangu mwenye upendo, nakupenda sana na ninaomba kwamba upendo wangu uwe daima mnyofu, wa kweli na kamili.  Nisaidie kuona namna zozote katika maisha yangu ambazo nashindwa kukupenda kwa moyo wangu wote.  Nakukabidhi maisha yangu bila kujibakizia chochote, Bwana mpendwa.  Yesu, nakutumainia.


Kushinda Vitisho

Alhamisi ya Wiki ya Thelathini ya Kipindi cha Kawaida

Baadhi ya Mafarisayo walimjia Yesu na kusema, “Ondoka, uache eneo hili kwa sababu Herode anataka kukuua.” Akajibu, “Nendeni mkamwambie huyo mbweha, ‘Tazama, ninafukuza pepo na kuponya leo na kesho, na siku ya tatu ninatimiza kusudi langu.’”  Luka 13:31-32

Mazungumzo haya kati ya Yesu na baadhi ya Mafarisayo yalikuwa ya kuvutia sana!  Inavutia kutazama matendo ya Mafarisayo na pia yale ya Yesu.

Mtu anaweza kuuliza kwa nini Mafarisayo walizungumza na Yesu kwa namna hii, wakimwonya kuhusu nia ya Herode.  Je, walikuwa na wasiwasi juu ya Yesu, na kwa hiyo walikuwa wakijaribu kumsaidia?  Huenda sivyo.  Badala yake, tunajua kwamba Mafarisayo wengi walikuwa na wivu na kijicho dhidi ya Yesu.  Katika hali hii, inaonekana kwamba walikuwa wakimwonya Yesu kuhusu ghadhabu ya Herode kama njia ya kujaribu kumtisha ili aondoke katika wilaya yao.  Bila shaka, Yesu hakutishwa.

Wakati mwingine tunapatwa na jambo hilohilo.  Nyakati fulani mtu anaweza kuja na kutusimulia porojo fulani zinazotuhusu, akijifanya anajaribu kutusaidia, ilhali kwa kweli hiyo ni njia ya hila ya kututisha ili kutujaza hofu au wasiwasi.

Jambo la msingi ni kuitikia tu kwa namna ile ambayo Yesu aliitikia alipokabiliwa na upumbavu na nia mbaya.  Yesu hakukubali kutishwa.  Hakusumbuliwa hata kidogo na nia mbaya ya Herode.  Badala yake, alijibu kwa namna ambayo, kwa maana fulani, iliwaambia Mafarisayo, “Msipoteze muda wenu kujaribu kunijaza hofu au wasiwasi.  Ninafanya kazi za Baba yangu, na hilo ndilo pekee ninalopaswa kulijali.”

Ni nini kinachokusumbua katika maisha?  Ni nini kinachokutisha?  Je, unaruhusu maoni, nia mbaya au porojo za wengine zikuvunje moyo?  Jambo pekee tunalopaswa kulijali ni kufanya mapenzi ya Baba wa Mbinguni.  Tunapofanya mapenzi Yake kwa kujiamini, tutakuwa pia na hekima na ujasiri tunaohitaji ili kukemea udanganyifu wote na vitisho vya kipuuzi katika maisha yetu.

Tafakari leo juu ya jinsi unavyojitoa kutimiza mapenzi ya Baba katika maisha yako.  Je, unatimiza mapenzi Yake?  Ikiwa ndivyo, je, unaona kwamba baadhi ya watu wanakuja na kujaribu kukuzuia?  Jitahidi kuwa na ujasiri uleule aliokuwa nao Yesu, na uendelee kuzingatia utume uliopewa na Mungu.

Bwana, kwa kweli ninayatumainia mapenzi Yako ya kimungu.  Ninatumainia mpango ulioniandalia, nami ninakataa kushawishiwa au kutishwa na upumbavu na nia mbaya za wengine.  Nipe ujasiri na hekima ili niendelee kukukazia macho katika mambo yote.  Yesu, nakutumainia.


Kumwalika Yesu

Ijumaa ya Wiki ya Thelathini ya Kipindi cha Kawaida

Siku moja ya sabato, Yesu alikwenda kula nyumbani kwa mmoja wa viongozi wa Mafarisayo, na watu waliokuwapo walikuwa wakimtazama kwa makini. Luka 14:1

Maneno haya, kutoka mwanzoni mwa Injili ya leo, yanafunua mambo mawili yanayostahili kutafakariwa.

Kwanza, Yesu alikwenda kula nyumbani kwa mmoja wa viongozi wa Mafarisayo. Hili halikuwa jambo dogo. Kwa kweli, yaelekea sana lilizua mazungumzo mengi miongoni mwa watu na Mafarisayo wengine. Linatuonyesha kwamba Yesu hana upendeleo. Hakuja kwa ajili ya maskini na wanyonge pekee. Alikuja pia kwa ajili ya kuongoka kwa matajiri na wenye mamlaka. Mara nyingi mno tunasahau ukweli huo ulio wazi. Yesu alikuja kwa ajili ya watu wote, anawapenda watu wote na anaitikia mialiko ya wote wanaotaka kuwa Naye katika maisha yao. Bila shaka, kifungu hiki pia kinaonyesha kwamba Yesu hakuogopa kuja nyumbani kwa kiongozi huyu wa Mafarisayo na kumpa yeye pamoja na wageni wake changamoto ili kuwahimiza wabadili mioyo yao.

Pili, kifungu hiki kinasema kwamba watu walikuwa “wakimwangalia kwa makini.” Labda baadhi yao walikuwa na udadisi tu na walitafuta jambo la kuzungumzia baadaye na rafiki zao. Lakini yaelekea sana wengine walikuwa wakimwangalia kwa makini kwa sababu walitaka kweli kumwelewa. Waliweza kutambua kwamba kulikuwa na jambo la pekee kuhusu Yesu na walitaka kumjua zaidi.

Mafundisho haya mawili yanapaswa kututia moyo tutambue kwamba Yesu anatupenda kweli na ataitikia utayari wetu wa kuupokea uwepo Wake katika maisha yetu.  Tunachohitaji kufanya ni kuomba na kuwa tayari kumpokea aje “kula” pamoja nasi.  Tunapaswa pia kujifunza kutokana na ushuhuda wa wale waliokuwa wakimtazama kwa makini.  Wanatuonyesha hamu njema tunayopaswa kuwa nayo ya kuendelea kumkazia Yesu macho.  Ingawa baadhi ya waliomtazama kwa makini walimgeuka na kumdhihaki, kulikuwa na wengine waliomtazama kwa makini na kumpokea Yesu pamoja na ujumbe Wake.

Tafakari leo kuhusu utayari wako wa kumwalika Yesu katika makao ya moyo wako na katika hali ya maisha yako. Jua kwamba atakubali kila mwaliko unaompa. Na Yesu anapokuja kwako, mwelekezee umakini wako wote. Angalia kwa makini yote anayosema na kutenda, na uruhusu uwepo Wake na ujumbe Wake viwe msingi wa maisha yako.

Bwana mkarimu sana, ninakualika kweli moyoni mwangu.  Ninakualika katika kila hali ya maisha yangu.  Tafadhali njoo ukae nami katika familia yangu.  Njoo ukae nami kazini, nikiwa kati ya marafiki, katika shida zangu, ninapokata tamaa, na katika mambo yote.  Nisaidie kuwa makini zaidi kwako na kwa mapenzi Yako, uniongoze kwenye yote uliyoyaandaa kwa ajili ya maisha yangu.  Yesu, nakutumainia.


Aibu Inayoletwa na Majivuno

Jumamosi ya Wiki ya Thelathini ya Kipindi cha Kawaida

“Unapoalikwa na mtu kwenye karamu ya arusi, usikae mezani mahali pa heshima. Huenda akawa amemwalika mgeni mwenye heshima zaidi kuliko wewe, naye mwenyeji aliyewaalika ninyi wawili anaweza kukujia na kusema, ‘Mpishe mtu huyu mahali pako,’ nawe hapo utaondoka kwa aibu kwenda kukaa mahali pa mwisho.” Luka 14:8-9

Kwa kuwasimulia mfano huu wale waliokuwa wakila pamoja Naye nyumbani kwa yule Farisayo, Yesu anagusa jambo lenye uzito mioyoni mwao.  Ni wazi kwamba miongoni mwa wasikilizaji Wake walikuwa wengi waliotafuta kuheshimiwa na wengine na waliojali sana sifa zao katika jamii.  Wazo la kuketi mahali pa heshima karamuni kisha kuaibishwa na mwenyeji kwa kuombwa kuhamia mahali pa chini lingewatia hofu.  Wale waliokuwa wametekwa na kutafuta hadhi katika jamii waliielewa vizuri aibu hiyo.

Yesu anatumia mfano huu wa kuaibisha kama njia ya kuonyesha wazi majivuno yao na hatari ya kuishi kwa majivuno ya namna hiyo. Anaendelea kusema, “Kwa maana kila anayejikweza atashushwa, lakini anayejinyenyekeza atakwezwa.”

Hata tukichunguza dhamiri zetu mara nyingi kadiri gani kuhusu majivuno, bado tunahitaji kuendelea kufanya hivyo. Kuna sababu ya majivuno kuitwa “Mama wa dhambi zote.” Majivuno huongoza kwenye kila dhambi nyingine na, kwa njia nyingi, ndiyo chanzo cha dhambi zote. Kwa hiyo, ikiwa tunataka kujitahidi kufikia ukamilifu maishani, tunapaswa kutafuta unyenyekevu wa kweli kila siku.

Unyenyekevu si kitu kingine ila kuyaona mambo jinsi yalivyo.  Mtu mnyenyekevu anajiona katika ukweli wa Mungu.  Hili linaweza kuwa gumu kufanya kwa sababu linatutaka tujione kuwa dhaifu na wenye kumtegemea Mungu.  Tunaweza kufanikisha mambo mengi ya kidunia kwa nguvu zetu wenyewe na kwa kufanya kazi kwa bidii.  Lakini hatuwezi kupata furaha na wema isipokuwa tuwe tayari kuukubali ukweli wa udhaifu wetu na wa kumtegemea Mungu kwa mambo yote.

Unyenyekevu pia husaidia kuitakasa mioyo yetu kutokana na jambo ambalo ni vigumu sana kuliacha. Majivuno hutufanya tutamani sana kuthaminiwa na wengine na kutegemea kuthaminiwa huko ili tuwe na furaha. Hiyo ni njia hatari kuifuata, kwa sababu hutuacha tukitegemea daima maoni ya wengine. Na mara nyingi mno, maoni ya wengine hutegemea vigezo vya uongo na vya kuangalia mambo kwa juu juu.

Tafakari leo kuhusu kiwango ambacho uko huru kutokana na maoni ya wengine yenye kupotosha na yasiyo ya kweli. Bila shaka, unahitaji kutafuta ushauri mara kwa mara kutoka kwa watu unaowajua na kuwapenda. Lakini ni lazima ujikubalie kumtegemea Mungu na Ukweli Wake pekee. Unapofanya hivyo, utakuwa umepiga hatua kubwa katika njia ya unyenyekevu wa kweli.

Bwana wa Ukweli, tafadhali unifanye kuwa mnyenyekevu.  Ondoa kiburi chote maishani mwangu ili niweze kukugeukia Wewe na kuyafuata mapenzi Yako pekee.  Nisaidie kujali tu Ukweli unaouweka na kuutumia kama kipimo pekee cha nafsi yangu.  Yesu, nakutumainia.

Yaliyomo


Pia Kinapatikana kama Kitabu chenye Jalada Laini & Kitabu cha Kielektroniki

Shiriki ukurasa huu: