Sw. Mimi nimewaona watu wakining’iniza rozari kwenye vioo vya kuangalia nyuma katika magari yao, na baadhi ya watu huzivaa shingoni. Je, ni sawa kufanya hivyo?
J. Kwanza kabisa, nitoe jibu rahisi kwa kusema kwamba nadhani mazoea haya ni sawa. Ninawajua watu wengi wenye ibada thabiti wanaompenda Bwana wetu na Mama Yake Mbarikiwa, ambao huning’iniza rozari kwenye vioo vya kuangalia nyuma vya magari yao. Kwao, hii ni njia ya kuudhihirisha upendo wao kwa Maria ili wote wauone. Jambo hilohilo linaweza kusemwa kuhusu wale wanaozivaa shingoni. Mtu akichagua kufanya mojawapo ya mambo haya, kuna uwezekano mkubwa kwamba anafanya hivyo kwa sababu ya ibada na upendo alio nao kwa Mama yetu Mbarikiwa. Ingawa sining’inizi rozari kwenye kioo changu wala siivai shingoni, huwa nayo mfukoni daima. Usiku, ninalala nikiwa nimeizungusha kwenye kifundo cha mkono wangu. Nafikiri kuwa na rozari karibu nasi ni sawa na kuvaa msalaba au skapulari, au kutundika picha takatifu chumbani mwetu. Rozari ni vitu vilivyobarikiwa na, kwa sababu hiyo, ni vizuri kuwa nazo karibu.
Ni lazima pia isemwe kwamba Rozari, kwanza kabisa, ni chombo cha sala na mojawapo ya sala bora zaidi tunazoweza kusali. Badala ya kuieleza Rozari kwa maneno yangu mwenyewe, niruhusu nikushirikishe baadhi ya nukuu ninazozipenda zaidi kutoka kwa watakatifu wakuu kuhusu rozari.
“Mtu yeyote anayesali Rozari yake kila siku hatapotoshwa kamwe. Hii ni kauli ambayo ningefurahi kuitia sahihi kwa damu yangu.” Mtakatifu Ludoviko de Montfort
“Kati ya sala zote, rozari ndiyo nzuri zaidi na yenye neema nyingi zaidi…ipende Rozari na uisali kila siku kwa ibada.” Papa Mtakatifu Pio X
“Jinsi ilivyo nzuri familia inayosali Rozari kila jioni.” Papa Mtakatifu Yohane Paulo II
“Rozari ndiyo sala ninayoipenda zaidi. Sala ya ajabu! Ya ajabu kwa urahisi wake na kina chake.” Papa Mtakatifu Yohane Paulo II
“Rozari ni hazina isiyokadirika thamani yake, iliyotokana na uvuvio wa Mungu.” Mtakatifu Ludoviko de Montfort
“Hakuna njia ya hakika zaidi ya kuiombea familia baraka za Mungu… kuliko kusali Rozari kila siku.” Papa Pio XII
“Rozari ndiyo aina bora kabisa ya sala na njia yenye ufanisi mkubwa zaidi ya kuufikia uzima wa milele. Ni dawa ya maovu yetu yote, mzizi wa baraka zetu zote. Hakuna njia bora zaidi ya kusali.” Papa Leo XIII
“Nipeni jeshi linalosali Rozari nami nitaushinda ulimwengu.” Papa Mwenyeheri Pio IX
Ikiwa mnatamani amani mioyoni mwenu, katika nyumba zenu na katika nchi yenu, kusanyikeni kila jioni kusali Rozari. Msiiache hata siku moja ipite bila kuisali, hata kama mmelemewa na mahangaiko na kazi nyingi.” Papa Pio XI
“Mama Yetu hajawahi kuninyima neema niliyoiomba kwa kusali Rozari.” Mtakatifu (Padre) Pio wa Pietrelcina
“Njia bora zaidi ya kusali ni kusali Rozari.” Mtakatifu Fransisko wa Sales
“Siku moja, kwa njia ya Rozari na Skapulari, Mama Yetu atauokoa ulimwengu.” Mtakatifu Dominiko
Maswali na Majibu Zaidi kuhusu Imani Katoliki
