Kiswahili

Siku ya Ishirini na Nane – Mikono na Miguu Yake


Toleo la Video

Mtafakari Yesu, aliyetupwa chini juu ya msalaba. Aliinyosha mikono Yake na kumtolea Baba Yake wa milele sadaka ya maisha Yake kwa ajili ya wokovu wetu. Walipigilia misumari mikononi na miguuni Mwake, kisha, wakiuinua msalaba, wakamwacha afe katika uchungu. (Kituo cha Kumi na Moja cha Njia ya Msalaba, cha Mtakatifu Alfonso Liguori)

Mama yetu Mbarikiwa alipokuwa amesimama mbele ya Msalaba wa Mwana wake, upendo ulimsukuma kuyaabudu majeraha katika mikono na miguu Yake mitakatifu. Alivutwa kuitazama misumari iliyomchoma Mwana wake walipoipigilia mikono Yake Msalabani. Ukatili ulioje. Bila huruma hata kidogo. Maumivu yaliyosababishwa na misumari hiyo yalikuwa makali mno. Mama yetu Mbarikiwa hakuweza kufanya lolote ila kutazama kwa upendo na kutafakari majeraha aliyojeruhiwa Mwana wake wa kimungu.

Kwa nini walimpigilia Yesu Msalabani? Alipigiliwa Msalabani ili kutimiza Maandiko. Nabii Isaya alisema, “Alichomwa kwa ajili ya dhambi zetu, alichubuliwa kwa ajili ya uovu wetu. Aliibeba adhabu inayotuletea uzima kamili, kwa majeraha yake tuliponywa” (Isaya 53:5).

“Kwa majeraha Yake tuliponywa.” Kauli yenye fumbo lililoje. Inakuwaje kwamba majeraha ya Yesu yanauletea ulimwengu uponyaji? Mama yetu Mbarikiwa alipokuwa akilitafakari fumbo hili kuu na kuyaabudu majeraha katika mikono na miguu ya Mwana wake, huenda alikumbuka sehemu iliyobaki ya unabii wa Isaya, “Sisi sote tulikuwa tumepotea kama kondoo, kila mmoja akifuata njia yake mwenyewe; Lakini BWANA aliweka juu yake hatia yetu sote. Ingawa alitendewa kwa ukatili, alijinyenyekeza wala hakufungua kinywa chake; Kama mwanakondoo anayepelekwa kuchinjwa au kondoo aliye kimya mbele ya wakataji wa manyoya, hakufungua kinywa chake” (Isaya 53:6-7).

Yesu aliukumbatia Msalaba na kukubali kwa hiari kuchomwa kwa ajili ya makosa yetu. Alijitwika matokeo ya dhambi zetu na kulipa gharama kwa kifo. Katika tendo hili la kuyatoa maisha Yake kwa hiari akiwa Mwanakondoo asiye na doa wala hatia, Aliiharibu sheria ya kifo na kuzigeuza dhambi na kifo kuwa uzima mpya.

Fumbo la mateso ya Yesu akiwa Mwanakondoo asiye na hatia ni la kina na linazidi uwezo wetu wa kufahamu. Mama yetu Mwenye Heri alilitafakari fumbo hili kuu la mateso moyoni mwake na alijua, kwa imani, kwamba kila jeraha na kila msumari vilileta neema isiyopimika ulimwenguni. Katika Mwanawe aliyesulubiwa, aliona athari za dhambi za ulimwengu. Lakini pia aliona dhambi ikiangamizwa kwa jinsi Mwanawe alivyoyakubali mateso kwa hiari akiwa hana hatia.

Mara nyingi sana tunashindwa kuelewa kwamba mateso na kifo cha Bwana wetu ni fumbo. Tunashindwa kufahamu na kushukuru kwa fumbo kuu la mateso Yake aliyoyapata bila hatia, ambayo yanatuweka huru.

Tafakari leo juu ya madonda ya Mwanakondoo wa Mungu asiye na hatia. Yatazame madonda Yake pamoja na Mama yetu Mwenye Heri. Yaone madonda Yake kuwa ndiyo gharama iliyolipwa kwa ajili ya dhambi zako. Uruhusu moyo wako ujazwe shukrani za dhati unapotafakari fumbo hili lisiloweza kufahamika kikamilifu.

Mama yangu mpendwa, imani yako pekee ndiyo iliyoweza kupenya fumbo la mateso, kama vile misumari ilivyopenya mikono na miguu ya Mwana wako wa kimungu. Upendo wako pekee ndio ulioweza kufahamu huruma na uponyaji vilivyotolewa kwa njia ya madonda ya Mwanao. Nivute nitazame pamoja nawe kwa namna hii, ili akili na moyo wangu viweze kupenya maana yake.

Mama yangu mpendwa, pia ninakutolea wewe na Mwanao majeraha yanayonitesa bila haki. Kamwe nisilalamike wala kuikwepa nafasi ya kujitoa kwa hiari na kukubali mateso kwa ajili ya uponyaji wa wengine. Nifundishe kuliiga fumbo hili kuu la Mwanao katika maisha yangu mwenyewe.

Yesu wangu uliyechomwa, mama Yako aliyatazama kwa upendo madonda ya mikono na miguu Yako. Aliona na kuamini uponyaji uliowezekana kwa Wewe kukubali kwa hiari ukatili huo. Nipe neema ninayohitaji ili nami niyatazame madonda Yako matakatifu na kupenya maana ya fumbo lake. Nakushukuru, Bwana mpendwa, kwa huruma tele uliyoimimina kutoka katika madonda Yako matakatifu.

Mama Maria, uniombee. Yesu, nakutumainia.

Siku ya Ishirini na Tisa – Yesu Anainuliwa Msalabani

Yaliyomo

Pia Kinapatikana kama Kitabu cha Kielektroniki & Kitabu Chenye Jalada Laini!

Shiriki ukurasa huu: