Kiswahili

Njia ya Msalaba

Njia ya Msalaba kama ilivyotungwa na Mtakatifu Alfonso Liguori:
Tazama pia Njia ya Msalaba kadiri ya Mtakatifu Fransisko wa Asizi

Sikiliza unaposali:

Sala ya Mwanzo:

WOTE: Bwana wangu, Yesu Kristo,

Umefunga safari hii ili kufa kwa ajili yangu kwa upendo usioelezeka;

nami nimekuacha mara nyingi sana bila shukrani. | Lakini sasa nakupenda kwa moyo wangu wote;

na, kwa sababu nakupenda, najuta kwa dhati kwa kuwa nimekukosea.

Nisamehe, Mungu wangu, na uniruhusu kuandamana Nawe katika safari hii.

Unakwenda kufa kwa kunipenda;

nami nataka, Mkombozi wangu mpendwa, kufa kwa kukupenda.

Yesu wangu, nitaishi na kufa nikiwa daima nimeungana Nawe.

 

Pale msalabani akidumu

Alisimama Mama mwenye huzuni akilia

Karibu na Yesu hadi mwisho


 Kituo cha Kwanza: Pilato Anamhukumu Yesu Kufa

K: Tunakuabudu, ee Kristo, na tunakusifu. (Piga goti)

W: Kwa kuwa kwa msalaba Wako mtakatifu umeukomboa ulimwengu. (Simama)

K: Tafakari jinsi Yesu Kristo, baada ya kupigwa mijeledi na kuvikwa taji ya miiba, alivyohukumiwa na Pilato bila haki afe msalabani. (Piga magoti)

W: Yesu wangu unayestahili kuabudiwa,

hakuwa Pilato;

la, ni dhambi zangu zilizokuhukumu Ufe.

Nakusihi, kwa mastahili ya safari hii yenye huzuni,

uisaidie roho yangu katika safari yake kuelekea umilele.

Nakupenda, Yesu mpendwa;

nakupenda kuliko ninavyojipenda mwenyewe.

Kwa moyo wangu wote ninatubu kwa kuwa nimekukosea.

Unijalie nikupende daima; kisha unitendee utakavyo.

(Baba Yetu, Salamu Maria, Atukuzwe Baba.)

 

Katika moyo wake, akishiriki huzuni Yake

Akistahimili uchungu Wake wote mkali

Hatimaye upanga umepenya


Kituo cha Pili: Yesu Anaupokea Msalaba Wake

K: Tunakuabudu, ee Kristo, na tunakusifu. (Piga goti)

W: Kwa kuwa kwa msalaba Wako mtakatifu umeukomboa ulimwengu. (Simama)

K: Tafakari jinsi Yesu alivyotembea katika njia hii akiwa na msalaba mabegani Mwake, akitufikiria sisi na kumtolea Baba Yake, kwa ajili yetu, kifo alichokuwa karibu kukipata. (Piga magoti)

W: Yesu wangu mpendwa kuliko wote,

Nayakubali kwa moyo wote mateso yote uliyonipangia hadi kufa.

Nakusihi, kwa mateso yote uliyoyapata katika kuubeba msalaba Wako,

unisaidie kuubeba wangu kwa amani Yako kamilifu na kwa kujisalimisha Kwako kikamilifu.

Nakupenda, Yesu, pendo langu;

Natubu kwa kuwa nimekukosea.

Usiniache kamwe nijitenge Nawe tena.

Unijalie nikupende daima; kisha unitendee utakavyo.

(Baba Yetu, Salamu Maria, Atukuzwe Baba.)

 

Ee, huzuni na uchungu vilikuwa vikubwa mno

Mama yule aliyebarikiwa mno,

Wa Mwana wa pekee


Kituo cha Tatu: Yesu Anaanguka Mara ya Kwanza

K: Tunakuabudu, ee Kristo, na tunakusifu. (Piga goti)

W: Kwa kuwa kwa msalaba Wako mtakatifu umeukomboa ulimwengu. (Simama)

V: Tafakari kuanguka kwa Yesu mara ya kwanza. Kupoteza damu kwa kupigwa mijeledi na kuvikwa taji la miiba kulikuwa kumemdhoofisha sana hata akawa hawezi kutembea vizuri; na bado ilimbidi kubeba mzigo huo mkubwa mabegani Mwake. Askari walipokuwa wakimpiga kikatili, alianguka mara kadhaa chini ya msalaba mzito. (Piga magoti)

W: Yesu wangu mpendwa, / haukuwa uzito wa msalaba / bali uzito wa dhambi zangu uliokufanya uteseke sana namna hiyo. / Kwa mastahili ya kuanguka huku kwa mara ya kwanza, / uniokoe nisianguke katika dhambi ya mauti. / Nakupenda, ee Yesu wangu, kwa moyo wangu wote; / nasikitika kwa kuwa nimekukosea. / Nisije nikakukosea tena kamwe. / Unijalie nikupende daima; kisha unitendee utakavyo.

(Baba Yetu, Salamu Maria, Atukuzwe Baba.)

 

Kristo ananing’inia juu katika mateso

Naye Mama akiwa chini anautazama uchungu

Wa Mwanawe mwenye utukufu anayekufa


Kituo cha Nne: Yesu Anakutana na Mama Yake Mwenye Uchungu

K: Tunakuabudu, ee Kristo, na tunakusifu. (Piga goti)

W: Kwa kuwa kwa msalaba Wako mtakatifu umeukomboa ulimwengu. (Simama)

K: Tafakari jinsi Mwana alivyokutana na Mama Yake njiani kwenda Kalvari. Yesu na Maria walitazamana, na macho yao yakawa kama mishale mingi iliyoijeruhi mioyo ile iliyopendana kwa upendo mwororo sana (Piga magoti)

R: Yesu wangu mwenye upendo mkuu, / kwa uchungu ulioupata katika mkutano huu, / unijalie neema ya kuwa na ibada ya kweli kwa Mama Yako mtakatifu sana. / Na wewe, Malkia wangu, uliyelemewa na huzuni, / uniombee nipate / kumbukumbu yenye huruma na ya kudumu ya mateso ya Mwana wako wa kimungu. / Nakupenda, Yesu, Mpenzi wangu, kuliko vitu vyote. / Natubu kwa kuwa nimekukosea. / Usiniruhusu nikukosee tena kamwe. / Unijalie nikupende daima; kisha unitendee utakavyo.

(Baba Yetu, Salamu Maria, Atukuzwe Baba.)

 

Je, kuna mtu ambaye hangelia,

Akimwona katika mateso makubwa namna hii

Mama mpendwa wa Kristo?


Kituo cha Tano: Simoni Anamsaidia Yesu Kuubeba Msalaba

K: Tunakuabudu, ee Kristo, na tunakusifu. (Piga goti)

W: Kwa kuwa kwa msalaba Wako mtakatifu umeukomboa ulimwengu. (Simama)

K: Tafakari jinsi Yesu alivyokuwa dhaifu na mchovu. Katika kila hatua alikuwa karibu kukata roho. Kwa kuhofia kwamba angekufa njiani, ilhali walitaka afe kifo cha aibu cha msalaba, walimlazimisha Simoni wa Kirene kusaidia kuubeba msalaba nyuma ya Bwana Wetu. (Piga magoti)

W: Yesu wangu mpendwa, / sitaukataa msalaba kama alivyofanya Simoni: / naukubali na kuukumbatia. / Nakikubali hasa kifo nilichopangiwa / pamoja na maumivu yote yanayoweza kuambatana nacho. / Nakiunganisha na kifo Chako / na nakutolea Wewe. / Umekufa kwa kunipenda mimi; / nitakufa kwa kukupenda Wewe na kukupendeza. / Unisaidie kwa neema Yako. / Nakupenda, Yesu, pendo langu; / natubu kwa kuwa nimekukosea. / Usiniache nikukosee tena kamwe. / Unijalie nikupende daima; kisha unitendee utakavyo.

(Baba Yetu, Salamu Maria, Atukuzwe Baba.)

 

Je, moyo wa mwanadamu waweza kujizuia

Kushiriki uchungu wake

Katika uchungu usioelezeka wa Mama huyo?


Kituo cha Sita: Veronika Anampa Yesu Utaji Wake

K: Tunakuabudu, ee Kristo, na tunakusifu. (Piga goti)

W: Kwa kuwa kwa msalaba Wako mtakatifu umeukomboa ulimwengu. (Simama)

V: Tafakari huruma ya mwanamke mtakatifu, Veronika. Alipomwona Yesu katika mateso makali namna hiyo, uso Wake ukiwa umeloa jasho na damu, alimpa utaji wake. Yesu alijifuta uso, akaacha kwenye kitambaa hicho sura ya uso Wake mtakatifu. (Piga magoti)

R: Yesu wangu mpendwa, / uso Wako ulikuwa mzuri kabla hujaanza safari hii; / lakini sasa hauonekani tena kuwa mzuri / na umeharibika kwa majeraha na damu. / Ole wangu, roho yangu pia ilikuwa nzuri hapo awali / ilipopokea neema Yako katika Ubatizo; / lakini tangu hapo nimeiharibu kwa dhambi zangu. / Wewe peke Yako, Mkombozi wangu, waweza kuirudishia uzuri wake wa zamani. / Fanya hivyo kwa mastahili ya mateso Yako; kisha unitendee utakavyo.

(Baba Yetu, Salamu Maria, Atukuzwe Baba.)

 

Akiwa amechubuliwa, amedhihakiwa, amelaaniwa na kudhalilishwa

Alimtazama Mwanawe mpendwa

Akiwa ameraruliwa mwili wote kwa mijeledi yenye damu.


Kituo cha Saba: Yesu Anaanguka Mara ya Pili

K: Tunakuabudu, ee Kristo, na tunakusifu. (Piga goti)

W: Kwa kuwa kwa msalaba Wako mtakatifu umeukomboa ulimwengu. (Simama)

V: Tafakari jinsi kuanguka kwa Yesu mara ya pili chini ya msalaba Wake kunavyoamsha upya maumivu katika majeraha yote ya kichwa na viungo vya Bwana wetu anayeteseka. (Piga magoti)

R: Yesu wangu mpole sana, / ni mara ngapi Umenisamehe; / nami ni mara ngapi nimeanguka tena na kuanza tena kukukosea! / Kwa mastahili ya kuanguka huku kwa mara ya pili, / unipe neema ya kudumu katika upendo Wako hadi kufa. / Unijalie nikukimbilie daima katika majaribu yangu yote. / Ninakupenda, Yesu, Pendo langu, kwa moyo wangu wote; / ninasikitika kwa kuwa nimekukosea. / Usiniache nikukosee tena kamwe. / Unijalie nikupende daima; kisha unitendee utakavyo.

(Baba Yetu, Salamu Maria, Atukuzwe Baba.)

 

Kwa ajili ya dhambi za taifa Lake mwenyewe

Alimwona akining’inia akiwa ameachwa peke Yake

Hata alipoitoa roho Yake.


Kituo cha Nane: Yesu Anasema na Wanawake

K: Tunakuabudu, ee Kristo, na tunakusifu. (Piga goti)

W: Kwa kuwa kwa msalaba Wako mtakatifu umeukomboa ulimwengu. (Simama)

V: Tafakari jinsi wanawake walivyolia kwa huruma walipomwona Yesu akiwa katika uchungu mkubwa na akichuruzika damu alipokuwa akitembea njiani. Yesu akawaambia, “Msinililie sana mimi, bali walilieni watoto wenu.” (Piga magoti)

R: Yesu wangu, uliyelemewa na huzuni, / ninazililia dhambi nilizokutendea / kwa sababu ya adhabu ninayostahili kwa ajili yake; / na zaidi sana, kwa sababu ya machukizo niliyokusababishia kwa dhambi hizo, / Wewe uliyenipenda kwa upendo usio na mipaka. / Ni upendo Wako, kuliko hofu ya moto wa milele, / unaonifanya nizililie dhambi zangu. / Yesu wangu, ninakupenda kuliko ninavyojipenda mwenyewe; / ninasikitika kwa kuwa nimekukosea. / Usiniruhusu nikukosee tena kamwe. / Unijalie nikupende daima; kisha unitendee utakavyo.

(Baba Yetu, Salamu Maria, Atukuzwe Baba.)

 

Ee Mama mwema! Chemchemi ya Upendo,

Iguse roho yangu kutoka juu

Ufanye moyo wangu upatane na wako.


Kituo cha Tisa: Yesu Anaanguka Mara ya Tatu

K: Tunakuabudu, ee Kristo, na tunakusifu. (Piga goti)

W: Kwa kuwa kwa msalaba Wako mtakatifu umeukomboa ulimwengu. (Simama)

V: Tafakari jinsi Yesu Kristo alivyoanguka mara ya tatu. Alikuwa amedhoofika sana, na ukatili wa watesi Wake ulikuwa umepita kiasi; walijaribu kuharakisha hatua Zake ingawa hakuwa na nguvu za kutosha hata za kusogea. (Piga magoti)

 

R: Yesu wangu uliyefedheheshwa, / kwa udhaifu ulioupata ulipokuwa ukienda Kalvari, / unipe nguvu za kutosha kushinda hofu yote ya maoni ya watu / na tamaa zangu zote mbaya zilizonifanya niudharau urafiki Wako. / Nakupenda, Yesu, Mpenzi wangu, kwa moyo wangu wote; / najuta kwa kuwa nimekukosea. / Usiniruhusu nikukosee tena kamwe. / Unijalie nikupende daima; kisha unitendee utakavyo.

(Baba Yetu, Salamu Maria, Atukuzwe Baba.)

 

Unijalie nihisi kama ulivyohisi

Uifanye roho yangu iwake na kuyeyuka

Kwa upendo wa Kristo, Bwana wangu.


Kituo cha Kumi:

Yesu Anavuliwa Mavazi Yake

K: Tunakuabudu, ee Kristo, na tunakusifu. (Piga goti)

W: Kwa kuwa kwa msalaba Wako mtakatifu umeukomboa ulimwengu. (Simama)

V: Tafakari jinsi Yesu alivyovuliwa nguo kwa nguvu na watesi Wake waliokuwa wakimwua. Nguo za ndani zilikuwa zimeshikamana na mwili Wake uliochanika kwa majeraha, nao askari walizivua kwa ukatili hata ngozi ikatoka pamoja nazo. Mwonee huruma Mwokozi wako aliyetendewa kwa ukatili namna hiyo, nawe umwambie: (Piga magoti)

R: Yesu wangu usiye na hatia, / kwa uchungu ulioupata ulipovuliwa mavazi Yako, / unisaidie kujivua kila mshikamano na vitu vya dunia / ili nikuelekezee Wewe upendo wangu wote, Wewe unayestahili sana upendo wangu. / Ninakupenda, ee Yesu, kwa moyo wangu wote; / ninasikitika kwa kukukosea wakati wowote uliopita. / Usiniache nikukosee tena kamwe. / Unijalie nikupende daima; kisha unitendee utakavyo.

(Baba Yetu, Salamu Maria, Atukuzwe Baba.)

 

Mama Mtakatifu, nichome hadi ndani

Katika moyo wangu fufua kila jeraha

Ya Mwokozi wangu aliyesulubiwa.


Kituo cha Kumi na Moja: Yesu Anapigiliwa Misumari Msalabani

K: Tunakuabudu, ee Kristo, na tunakusifu. (Piga goti)

W: Kwa kuwa kwa msalaba Wako mtakatifu umeukomboa ulimwengu. (Simama)

V: Tafakari jinsi Yesu alivyotupwa juu ya msalaba, akanyosha mikono Yake na kumtolea Baba Yake wa milele sadaka ya maisha Yake kwa wokovu wetu. Walipigilia misumari mikono na miguu Yake, kisha wakainua msalaba na kumwacha afe kwa uchungu. (Piga magoti)

R: Yesu wangu uliyedharauliwa, / upigilie moyo wangu msalabani / ili ubaki daima hapo kukupenda na usikuache tena kamwe. / Ninakupenda kuliko ninavyojipenda; / ninasikitika kwa kuwa nimekukosea. / Usiniruhusu nikukosee tena kamwe. / Unijalie nikupende daima; kisha unitendee utakavyo.

(Baba Yetu, Salamu Maria, Atukuzwe Baba.)

 

Nijalie kushiriki nawe maumivu Yake,

Yeye aliyeuawa kwa ajili ya dhambi zetu zote,

Yeye aliyekufa kwa mateso kwa ajili yangu.


Kituo cha Kumi na Mbili: Yesu Anakufa Msalabani

K: Tunakuabudu, ee Kristo, na tunakusifu. (Piga goti)

W: Kwa kuwa kwa msalaba Wako mtakatifu umeukomboa ulimwengu. (Simama)

V: Tafakari jinsi Yesu wako, baada ya saa tatu za mahangaiko makali msalabani, hatimaye anavyolemewa na mateso na, akijiachia kwa uzito wa mwili Wake, anainamisha kichwa Chake na kufa. (Piga magoti)

R: Yesu wangu unayekata roho, / naubusu kwa ibada msalaba ambao juu yake ungekufa kwa kunipenda. / Kwa sababu ya dhambi zangu, nastahili kufa kifo cha kutisha; / lakini kifo Chako ndicho tumaini langu. / Kwa mastahili ya kifo Chako, / unipe neema ya kufa nikiikumbatia miguu Yako na kuwaka kwa upendo Kwako. / Naiweka roho yangu mikononi Mwako. / Nakupenda kwa moyo wangu wote. / Najuta kwa kuwa nimekukosea. / Usiniache nikukosee tena kamwe. / Unijalie nikupende daima; kisha unitendee utakavyo.

(Baba Yetu, Salamu Maria, Atukuzwe Baba.)

 

Nijalie kuunganisha machozi yangu na yako,

Nikimwombolezea Yeye aliyehuzunika kwa ajili yangu,

Siku zote nitakazoishi.


Kituo cha Kumi na Tatu:

Yesu Anashushwa Msalabani

K: Tunakuabudu, ee Kristo, na tunakusifu. (Piga goti)

W: Kwa kuwa kwa msalaba Wako mtakatifu umeukomboa ulimwengu. (Simama)

V: Tafakari jinsi Bwana wetu, baada ya kufa, alivyoshushwa msalabani na wanafunzi Wake wawili, Yosefu na Nikodemo, na kuwekwa mikononi mwa Mama Yake mwenye huzuni. Alimpokea kwa upendo mwororo usioelezeka, akamkumbatia kifuani pake. (Piga magoti)

R: Ee Mama wa Huzuni, / kwa upendo ulio nao kwa Mwana wako, / unikubali kuwa mtumishi wako na uniombee Kwake. / Na Wewe, Mkombozi wangu, kwa kuwa umekufa kwa ajili yangu, / uniruhusu nikupende, / kwa maana ninakutamani Wewe tu wala si kitu kingine. / Ninakupenda, Yesu, Pendo langu, / nami ninasikitika kwa kuwa nimekukosea. / Usiniache nikukosee tena kamwe. / Unijalie nikupende daima; kisha unitendee utakavyo.

(Baba Yetu, Salamu Maria, Atukuzwe Baba.)

 

Kukaa nawe karibu na msalaba,

Hapo kulia na kusali pamoja nawe,

Ndilo pekee ninalokuomba unijalie.


Kituo cha Kumi na Nne:

Yesu Anawekwa Kaburini

K: Tunakuabudu, ee Kristo, na tunakusifu. (Piga goti)

W: Kwa kuwa kwa msalaba Wako mtakatifu umeukomboa ulimwengu. (Simama)

V: Tafakari jinsi wanafunzi walivyouchukua mwili wa Yesu kwenda kuuzika, huku Mama Yake mtakatifu akiandamana nao na kuulaza kaburini kwa mikono yake mwenyewe. Kisha wakalifunga kaburi na wote wakaondoka. (Piga magoti)

R: Ee Yesu wangu uliyezikwa, / ninalibusu jiwe linalokufungia kaburini. / Lakini Wewe ulifufuka kwa utukufu siku ya tatu. / Ninakuomba kwa ufufuko Wako nifufuliwe kwa utukufu siku ya mwisho, / ili niungane Nawe mbinguni, nikusifu na kukupenda milele. / Ninakupenda, Yesu, nami ninatubu kwa kuwa nimekukosea. / Unijalie nikupende daima; kisha unitendee utakavyo.

(Baba Yetu, Salamu Maria, Atukuzwe Baba.)

 

Ee Bikira mbarikiwa kuliko mabikira wote!

Sikiliza ombi langu la upendo:

Nijalie kushiriki huzuni yako ya kimungu.


Sala kwa Yesu Kristo Aliyesulubiwa

Yesu wangu mwema na mpendwa,

Ninapiga magoti mbele Yako,

nikikuomba kwa bidii kubwa

uchore moyoni mwangu

imani, matumaini na mapendo yaliyo na kina na uhai,

kwa toba ya kweli kwa dhambi zangu,

na azimio thabiti la kurekebisha makosa yangu.

Ninapotafakari madonda Yako matano,

na kuyatafakari kwa makini

kwa huruma kubwa na huzuni,

nakumbuka, Yesu mwema,

maneno aliyosema Nabii Daudi

zamani sana kukuhusu Wewe:

“Wametoboa mikono Yangu na miguu Yangu;

wamehesabu mifupa Yangu yote.”

 

Tazama sala na nyenzo kwa ajili ya Kwaresima


Tafakari kuhusu mawazo na moyo wa Mama yetu Mbarikiwa alipokuwa amesimama kwa uaminifu chini ya Msalaba wa Yesu, Mwana wake.

Siku 40 Chini ya Msalaba:
Mtazamo wa Upendo kutoka Moyoni mwa Mama Yetu Mbarikiwa


Video inayopendekezwa kwa ajili ya

Njia ya Msalaba

Kadiri ya Mtakatifu Alfonso Liguori

Shiriki ukurasa huu: