Kiswahili

Maadili Yangu ya Kikatoliki! Kipindi cha Kwanza cha Kujifunza

Mimi Ni Nani?

Pakua kipindi: PDF – Toleo linaloweza kuhaririwa

Maandalizi Kabla ya Mkutano
Washiriki waombwe kusoma Utangulizi na Sura ya Kwanza ya Maadili Yangu ya Kikatoliki! kabla ya mkutano huu.

Dakika 5 – Kukusanyika
Wakati huu wa mwanzo wa kukusanyika ni nafasi tu ya kila mtu kufika na kukutana na wengine. Wakati huu wa mwanzo wa kukusanyika, kiongozi ahakikishe kwamba ana taarifa zote za mawasiliano za washiriki. Vitambulisho vya majina vinaweza kusaidia.

Dakika 5 – Kutambulishana
Kama mwenyeji, wakusanye wote pamoja na kuwakaribisha. Eleza machache kuhusu wewe mwenyewe, kisha mpe kila mtu nafasi ya kujitambulisha kwa ufupi.

Dakika 5-10 – Sala ya kufungua na Maandiko Matakatifu
Wote wanaketi kimya wakati kiongozi anapoanza kwa Ishara ya Msalaba, kisha anawaalika kukaa kimya kwa muda kwa namna ifuatayo:

“Tutulie tunapoanza pamoja kujifunza maadili yetu adhimu ya Kikatoliki. ‘Bwana, tunapoketi hapa kwa dakika moja katika ukimya, umsaidie kila mmoja wetu kuleta Kwako maswali yake, mahangaiko yake, hofu zake na furaha zake. Utusaidie, katika wakati huu wa ukimya, kuisikiliza kwa makini sauti Yako ya upole inayosema nasi, ikituongoza na kutuita tuwe na imani ya kina zaidi.'”

Kaeni kimya kwa takribani dakika moja mkiwa mmefumba macho ili kila mmoja aweze kuzungumza na Bwana wetu kuhusu mahangaiko na masuala yake binafsi yanayomtia wasiwasi.

Kiongozi anasoma mwaliko ufuatao:

Tulitafakari Neno la Mungu. Tutafakari safari yetu wenyewe ya imani kwa kujiuliza maswali yafuatayo: Je, ninaamini? Imani yangu ina kina gani? Je, niko tayari kumruhusu Mungu aseme nami? Je, niko tayari kulipokea Neno la Mungu na kuiruhusu kweli ya Mungu iingie ndani yangu kwa kina zaidi? Je, niko tayari kuruhusu imani hii mpya ibadilishe maisha yangu?

Kiongozi wa kipindi anasoma Maandiko Matakatifu yafuatayo kwa moyo wa sala, andiko moja baada ya jingine, akitua kwa takribani sekunde 30 kati ya mstari mmoja na mwingine:

Mathayo 5:3-12: Heri walio maskini wa roho, maana ufalme wa mbinguni ni wao.
Heri wanaoomboleza, maana watafarijiwa.
Heri walio wapole, maana watairithi dunia.
Heri wenye njaa na kiu ya haki, maana watashibishwa.
Heri wenye huruma, maana watapata huruma.
Heri wenye moyo safi, maana watamwona Mungu.
Heri wapatanishi, maana wataitwa wana wa Mungu.
Heri wanaodhulumiwa kwa ajili ya haki, maana ufalme wa mbinguni ni wao.
Heri ninyi watu wanapowatukana na kuwadhulumu na kusema kila aina ya uovu dhidi yenu kwa uongo kwa ajili yangu.
Furahini na kushangilia, maana thawabu yenu ni kubwa mbinguni.

1 Wakorintho 13:1-8: Nikisema kwa lugha za wanadamu na za malaika lakini sina upendo, mimi ni kama gongo linalovuma au upatu unaolia. Na nikiwa na kipaji cha unabii na kuelewa mafumbo yote na maarifa yote; nikiwa na imani yote kiasi cha kuhamisha milima lakini sina upendo, mimi si kitu. Nikitoa vyote nilivyo navyo, na nikiukabidhi mwili wangu ili nipate kujisifu lakini sina upendo, sifaidiki na chochote. Upendo una subira, upendo una fadhili. Hauna wivu, (upendo) haujionyeshi kwa majivuno, haujivuni, hauna utovu wa adabu, hautafuti masilahi yake wenyewe, haukasiriki upesi, hauweki kinyongo kwa mabaya yaliyotendewa, haufurahii uovu bali hufurahi pamoja na ukweli. Huvumilia yote, huamini yote, hutumaini yote, hustahimili yote. Upendo haushindwi kamwe.

Warumi 5:18-21: Kwa kumalizia, kama vile kwa kosa moja hukumu ya adhabu ilivyowafikia wote, vivyo hivyo kwa tendo moja la haki kuondolewa hatiani na uzima viliwafikia wote. Kwa maana kama vile kwa kutotii kwa mtu mmoja wengi walivyofanywa wenye dhambi, vivyo hivyo kwa kutii kwa mmoja wengi watafanywa wenye haki. Sheria iliingia ili makosa yaongezeke, lakini pale dhambi ilipoongezeka, neema ilifurika zaidi sana, ili, kama vile dhambi ilivyotawala katika mauti, neema nayo itawale kwa njia ya kuhesabiwa haki na kuleta uzima wa milele kwa njia ya Yesu Kristo Bwana wetu.

Kisha kiongozi aseme: Tukae kimya kwa muda mfupi tukitafakari maneno haya. (dakika moja ya ukimya)ย ย 

Kiongozi anawaalika wote kusali huku akisali sala ifuatayo kwa sauti:

Bwana Mungu wetu, tunakushukuru kwa hadhi uliyomjalia kila mmoja wetu, ukituwezesha kuitwa wana na binti Zako. Utusaidie daima kuitambua hadhi hiyo na kuikubali kwa moyo wote.

Bwana, utusaidie pia kuingia kwa undani zaidi katika utakatifu wa dhamiri zetu na kukutana Nawe humo ndani kabisa. Utusaidie kukuchagua Wewe na mapenzi Yako matakatifu katika mambo yote na kuendelea kuachana na kila dhambi.

Bwana, tunakuomba utufundishe Ukweli ndani ya dhamiri zetu. Utufundishe Wewe ni nani na yote uliyotuambia.

Muda wa sala unahitimishwa kwa wote kukiri Kanuni ya Imani ya Mitume:

Nasadiki kwa Mungu, Baba mwenyezi, Muumba mbingu na nchi; na kwa Yesu Kristo, Mwanawe pekee, Bwana wetu: aliyetungwa kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, akazaliwa na Bikira Maria; akateswa kwa mamlaka ya Ponsyo Pilato, akasulubiwa, akafa, akazikwa. Akashuka kuzimu; siku ya tatu akafufuka katika wafu; akapaa mbinguni, ameketi kuume kwa Mungu Baba mwenyezi; kutoka huko atakuja kuwahukumu wazima na wafu. Nasadiki kwa Roho Mtakatifu, Kanisa takatifu katoliki, ushirika wa watakatifu, maondoleo ya dhambi, ufufuko wa mwili, na uzima wa milele. Amina.

Dakika 45-50 – Maswali ya majadiliano
Kila mtu aalikwe kushirikisha jambo au kuuliza swali akipenda kuhusu maswali au vichocheo vya majadiliano vilivyo hapa chini.ย  Pitia swali moja baada ya jingine, na umpe kila mtu nafasi ya kusema jambo akipenda.ย  Epuka kuruhusu mtu mmoja au wawili kutawala majadiliano.ย  Pokezaneni kwa kufuata mzunguko, wala msiogope kushirikisha mawazo yenu!ย  Mawazo yako yanaweza kumsaidia mtu mwingine kuelewa mada hizi.ย  Huenda kabisa swali lako likawa swali lilelile alilo nalo mtu mwingine.ย  Baadhi ya maswali yaliyo hapa chini yatakualika kushirikisha mambo ya maisha yako binafsi; maswali mengine yatakualika kuwashirikisha wengine yale uliyosoma katika sura inayohusika na majadiliano haya.ย  Lengo ni kushirikishana mambo ya maisha yetu binafsi na kuhakikisha kwamba imani ya Kanisa letu inaelezwa kwa uwazi na kueleweka na wote.

  1. Unaupata wapi utambulisho wako? Watu wengi huupata wapi utambulisho wao? Mara nyingi tunaupata utambulisho wetu katika mambo ya juujuu zaidi, kama vile mwonekano wetu, mafanikio yetu, makundi ya watu tunaoshirikiana nao, na kadhalika. Tunapaswa kuupata wapi utambulisho wetu? Jadilianeni kuhusu jambo hili.
  2. Heri Nane zinatuita kuwa wale tulioumbwa kuwa, kwa ukamilifu wa hali ya juu kabisa. Someni baadhi ya Heri Nane na mjadili jinsi ilivyo rahisi au vigumu kuziishi.
  3. Uhuru wa binadamu ni muhimu kwa namna tunavyoishi.ย  Ikiwa hatuko huru kabisa, basi hatuwezi kuwa watu tulioumbwa kuwa.ย  Baadhi ya mambo yanayoathiri uhuru wetu ni haya: kutokujua, kulazimishwa, hofu, na mambo mengine ya kisaikolojia au kijamii.ย  Jadilini mambo haya na athari yanazoweza kuwa nazo kwetu na kwa namna tunavyofanya maamuzi maishani.
  4. Uadilifu wa tendo huamuliwa na mambo matatu: 1) kile kinachochaguliwa kufanywa; 2) lengo linalokusudiwa au nia; 3) mazingira ya tendo.ย  Jadilini kwa ufupi kama kikundi vyanzo hivi vitatu vya uadilifu wa tendo na jaribuni kutoa mifano ya kila kimoja.
  5. Jadilianeni kuhusu tofauti kati ya kitu tunachoweza kukiita Chema (C kubwa) na chema (c ndogo).
  6. Misukumo ya ndani, hisia na mihemko vina nafasi gani katika maisha yetu kuhusiana na maamuzi tunayofanya kuhusu mema na mabaya?
  7. Kuielewa dhamiri ni msingi wa kufanya maamuzi ya kimaadili na wa kuelewa sisi ni nani.ย  Jadilini uelewa wenu wa dhamiri kwa kufuata vichwa vifuatavyo:
    1. Dhamiri kama patakatifu pa siri ndani yetu, ambamo tunakuwa peke yetu na Mungu.
    2. Dhamiri iliyopotoka kwa kosa la mtu.
    3. Dhamiri iliyopotoka bila kosa la mtu.
  8. Fadhila kuu nne, fadhila tatu za kimungu, na vipaji saba vya Roho Mtakatifu, vyote hutusaidia kuishi maisha mema ya kimaadili.ย  Shirikishaneni tafakari zozote mlizo nazo baada ya kusoma kuhusu mambo haya.ย  Shirikishaneni jambo lolote ambalo huenda limewagusa kwa namna ya pekee.
  9. Dhambi: shirikishaneni mawazo yenu ya awali kuhusu sehemu inayozungumzia dhambi.ย  Ni jambo gani lililowagusa kwa namna ya pekee?
  10. Shirikishaneni hasa kuhusu tofauti kati ya dhambi nyepesi na dhambi ya mauti.ย  Jaribuni kujadili tofauti hiyo kwa uwazi.ย  Anzeni kwa kujadili masharti yafuatayo ya dhambi ya mauti:
    1. Jambo zito
    2. Ujuzi kamili
    3. Ridhaa kamili ya utashi

Dakika 20 – Tafakari za Mwisho na kushirikishana
Mpe kila mtu nafasi kwa zamu ya kushirikisha jambo ambalo huenda limemgusa zaidi katika majadiliano au lililomchanganya zaidi, ili apate ufafanuzi au ufahamu zaidi kutoka kwa wengine.

Dakika 5 – Sala ya Kuhitimisha
Kiongozi anaanza kwa Ishara ya Msalaba na kuwaalika wote kukaa kimya kwa dakika moja, wakiwa wamefumba macho. Kila mtu atafakari yale yaliyojadiliwa, hasa jambo lililomgusa zaidi.

Kisha kiongozi anasali sala ifuatayo:

Bwana Mungu, utusaidie daima kupata utambulisho wetu wa kweli katika kuwa wana na binti Zako.ย  Utusaidie kutambua kwamba tumeumbwa kwa mfano Wako na kuikubali hadhi inayotokana na utambuzi huo.

Bwana, utusaidie daima kujitahidi kuishi Heri na fadhila katika maisha yetu.ย  Tunapoitambua miito hii mitukufu, tuweze kuiishi kikamilifu ili kufikia furaha ya kweli.

Bwana Mungu, wakati mwingine tunatenda dhambi na kujitenga Nawe.ย  Wakati mwingine tunashindwa kuishi kulingana na wito wetu mtukufu maishani.ย  Katika nyakati hizo, utusaidie daima kuachana na dhambi na kurudi Kwako.ย  Daima tutumainie huruma na neema Yako ya kimungu.

Yesu, tunakutumainia.

Kisha kiongozi anawaalika wote waliopo kutoa sala zao wenyewe kwa namna ifuatayo (Angalizo: Hili linaweza kufanywa kwa sauti, lakini huenda ikafaa zaidi lifanywe kimya kimya, kadiri kiongozi atakavyoona inafaa):

Sasa kila mmoja wetu alete mahangaiko yake binafsi mbele ya Bwana wetu, akitumaini kwamba Yeye anatusikia na anajua yote tunayohitaji.ย  Tumkabidhi sala hizi tukiwa na tumaini kamili kwamba anatamani kushika usukani.

(Kaeni kimya kwa dakika moja ili kila mtu azungumze na Mungu kuhusu mahitaji yake binafsi).

Kisha kiongozi anawaalika wote kuhitimisha kwa kusali Baba Yetu, Salamu Maria na Atukuzwe Baba.

Yaliyomo katika Vipindi vya Mafunzo

Shiriki ukurasa huu: