Liturujia Takatifu
Pakua kipindi: PDF – Toleo linaloweza kuhaririwa
Maandalizi kabla ya mkutano
Washiriki waombwe kusoma Utangulizi na Sura ya Kwanza ya kitabu Ibada Yangu ya Kikatoliki! kabla ya mkutano huu.
Dakika 5 – Kukusanyika
Wakati huu wa awali wa kukusanyika ni nafasi tu ya kila mmoja kuwasili na kukutana na wengine. Katika wakati huu wa awali wa kukusanyika, kiongozi ahakikishe kwamba ana taarifa zote za mawasiliano za washiriki. Vitambulisho vya majina vinaweza kusaidia.
Dakika 5 – Kujitambulisha
Kama mwenyeji, wakusanye wote pamoja na uwakaribishe. Eleza machache kukuhusu, kisha mpe kila mtu nafasi kwa zamu ajitambulishe kwa kifupi.
Dakika 5-10 – Sala ya kufungua na Maandiko Matakatifu
Wote wanaketi kimya wakati kiongozi anapoanza kwa Ishara ya Msalaba, kisha anawaalika kukaa kimya kwa muda kwa namna ifuatayo:
“Tutulie tunapoanza pamoja kujifunza kuhusu ibada yetu tukufu ya Kikatoliki. ‘Bwana, tunapoketi hapa kwa dakika moja katika ukimya, umsaidie kila mmoja wetu kuleta Kwako maswali yake, mahangaiko yake, hofu zake na furaha zake. Utusaidie, katika wakati huu wa ukimya, kuisikiliza kwa makini sauti Yako ya upole inayosema nasi, inayotuongoza na kutuita tuwe na imani ya kina zaidi.'”
Kaeni kimya kwa takribani dakika moja mkiwa mmefumba macho ili kila mmoja aweze kuzungumza na Bwana wetu kuhusu mahangaiko na masuala yake binafsi yanayomtia wasiwasi.
Kiongozi anasoma mwaliko ufuatao:
Tulitafakari Neno la Mungu. Tutafakari safari yetu wenyewe ya imani kwa kujiuliza maswali yafuatayo: Je, ninaamini? Imani yangu ina kina gani? Je, niko tayari kumruhusu Mungu aseme nami? Je, niko tayari kulipokea Neno la Mungu na kuiruhusu kweli ya Mungu iingie ndani yangu kwa kina zaidi? Je, niko tayari kuruhusu imani hii mpya ibadilishe maisha yangu?
Kiongozi wa kipindi anasoma Maandiko Matakatifu yafuatayo kwa moyo wa sala, andiko moja baada ya jingine, akitua kwa takribani sekunde 30 kati ya mstari mmoja na mwingine:
Mathayo 22:37: “Mwalimu, ni amri ipi katika sheria iliyo kuu kuliko zote?” Akamwambia, “Mpende Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote na kwa akili yako yote. Hii ndiyo amri kuu na ya kwanza…”
Waefeso 1:9-12: Ametujulisha fumbo la mapenzi Yake kulingana na wema Wake aliouweka ndani ya Kristo kuwa mpango wa utimilifu wa nyakati, wa kuvikusanya vitu vyote katika Kristo, vilivyo mbinguni na vilivyo duniani. Ndani Yake sisi pia tulichaguliwa, tukiwa tumekusudiwa tangu awali kulingana na azimio la Yeye anayetimiza mambo yote kufuatana na nia ya mapenzi Yake, ili sisi tuliokuwa wa kwanza kumtumainia Kristo tuwe kwa ajili ya sifa ya utukufu Wake.
Yohane 17:4-10: Nimekutukuza duniani kwa kutimiza kazi uliyonipa niifanye. Sasa unitukuze, Baba, pamoja Nawe, kwa ule utukufu niliokuwa nao pamoja Nawe kabla ya ulimwengu kuwako. “Nimewafunulia jina Lako wale ulionipa kutoka ulimwenguni. Walikuwa Wako, Nawe ukanipa, nao wamelishika neno Lako. Sasa wanajua ya kuwa kila kitu ulichonipa kinatoka Kwako, kwa sababu maneno uliyonipa nimewapa wao, nao wameyapokea na kuelewa kweli kwamba nilitoka Kwako, na wameamini kwamba Wewe ulinituma. Ninawaombea hao. Siuombei ulimwengu bali wale ulionipa, kwa sababu ni Wako, na vyote vilivyo Vyangu ni Vyako, na vyote vilivyo Vyako ni Vyangu, nami nimetukuzwa ndani yao…“
Kisha kiongozi anasema: Tukae kimya kwa muda mfupi tukiyatafakari maneno haya. (dakika moja ya ukimya).
Kiongozi anawaalika wote kusali sala ifuatayo huku akiisali kwa sauti:
Bwana Yesu, nijifunze kukupenda katika mambo yote na kuliko vitu vyote. Nikupende kwa akili yangu yote, moyo wangu wote, roho yangu yote na nguvu zangu zote.
Bwana, ninapoanza kujifunza kuhusu ibada, unisaidie kuyachunguza maisha yangu mwenyewe ya sala na ibada. Unisaidie kutazama kwa unyofu jinsi ninavyoadhimisha Sakramenti na kutambua namna ninavyoweza kushiriki kikamilifu zaidi katika zawadi hizi.
Bwana, unanijia kwa undani mkubwa na kwa unyenyekevu, ukiwa umejificha ndani ya Liturujia. Niwe na macho ya imani ya kweli ili niweze kukutambua na kukupenda katika nyakati hizi za ibada.
Bwana, kukuabudu Wewe kuyatawale maisha yangu yote na kunijaze upendo wa kina zaidi kwa wengine. Kukuabudu Wewe kuujaze moyo wangu na roho yangu upendo kwa wengine ili niweze kuwa chombo Chako chenye ufanisi zaidi ulimwenguni.
Yesu, nakutumainia.
Wakati wa sala unahitimishwa kwa wote kukiri Imani ya Mitume:
Nasadiki kwa Mungu, Baba mwenyezi, Muumba mbingu na nchi; na kwa Yesu Kristo, Mwanawe pekee, Bwana wetu: aliyetungwa kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, akazaliwa na Bikira Maria; akateswa kwa mamlaka ya Ponsyo Pilato, akasulubiwa, akafa, akazikwa. Akashuka kuzimu; siku ya tatu akafufuka katika wafu; akapaa mbinguni, ameketi kuume kwa Mungu Baba mwenyezi; kutoka huko atakuja kuwahukumu wazima na wafu. Nasadiki kwa Roho Mtakatifu, Kanisa takatifu katoliki, ushirika wa watakatifu, maondoleo ya dhambi, ufufuko wa mwili, na uzima wa milele. Amina.
Dakika 45-50 – Maswali ya majadiliano
Kila mtu aalikwe kushirikisha jambo au kuuliza swali akipenda kuhusu maswali au vichocheo vya majadiliano vilivyo hapa chini. Pitia swali moja baada ya jingine, na umpe kila mtu nafasi ya kusema jambo akipenda. Epuka kuruhusu mtu mmoja au wawili kutawala majadiliano. Pokezaneni kwa kufuata mzunguko, wala msiogope kushirikisha mawazo yenu! Mawazo yako yanaweza kumsaidia mtu mwingine kuelewa mada hizi. Huenda kabisa swali lako likawa swali lilelile alilo nalo mtu mwingine. Baadhi ya maswali yaliyo hapa chini yatakualika kushirikisha mambo ya maisha yako binafsi; maswali mengine yatakualika kuwashirikisha wengine yale uliyosoma katika sura inayohusika na majadiliano haya. Lengo ni kushirikishana mambo ya maisha yetu binafsi na kuhakikisha kwamba imani ya Kanisa letu inaelezwa kwa uwazi na kueleweka na wote.
- Ni nini unachokiona kuwa “chenye thamani isiyopimika?” Orodha yake ina mambo gani? Anza na mambo yasiyohusiana moja kwa moja na imani, kisha, baada ya kuandaa orodha, ilinganishe na orodha ambayo ingejumuisha mambo yenye thamani isiyopimika katika maisha yetu ya imani, sala na ibada.
- Ungeelezaje maana ya “fumbo?” Jadili kwanza “fumbo” kwa ujumla, bila kuingiza imani katika ufafanuzi huo kwa sasa.
- Sasa, ni kwa namna gani Liturujia ni “Mysterium Fidei?” Fumbo la Imani? Jadili jambo hili kwa kina, ukijaribu kuelewa zaidi njia nyingi ambazo maisha yetu, imani yetu na ibada yetu zinajumuisha mafumbo mengi yasiyohesabika ya imani.
- Liturujia ni “tendo la Mungu” na pia “tendo la Kanisa.” Jadili na kufafanua namna ambazo Liturujia ni:
- Tendo la Mungu – Ina maana gani kusema kwamba Liturujia ni tendo la Mungu kwa 100%? Hilo ni kweli kwa namna gani?
- Tendo la Kanisa – Ina maana gani kusema kwamba Liturujia ni tendo la Kanisa kwa 100%? Hilo ni kweli kwa namna gani?
- Je, Liturujia inachosha? Hapana, hili si swali la mtego (ingawa, kwa kiasi fulani, ndivyo lilivyo). Jadili jambo hili kwa makini, ukitumia utaratibu ufuatao:
- Je, nyakati fulani Liturujia inachosha? Ndiyo au hapana?
- Je, hilo lina umuhimu? Je, kuna tofauti yenye umuhimu ikiwa inachosha au haichoshi? Jaribu kutumia muda kiasi kulijadili hili. Yaelekea kutakuwa na maoni mengi.
- Je, lengo la Liturujia (Misa Takatifu au ibada nyingine yoyote ya kiliturujia) linapaswa kuwa kutuburudisha, kwa kuzingatia kwamba hatuwezi kuwa makini kwa muda mrefu? Je, tunapaswa kujaribu kushindana na Hollywood na aina nyingine za burudani za kisasa? Kuna hatari gani katika kufanya hivyo?
- Je, kuna faida zozote za kuifanya Liturujia iendelee “kuchosha” kwa vigezo vya ulimwengu? Mtakatifu anawezaje kufaidika na Liturujia zenye ukavu zaidi wa kihisia na zenye taadhima?
- Ni nini kinachopaswa kuwa kiini halisi cha Liturujia? Sisi kama Kanisa tunawezaje kujitahidi kwa namna bora zaidi kufikia lengo hilo?
- Liturujia ina uhusiano gani na imani yetu? Uhusiano huo ni upi?
- Jadilianeni kuhusu namna Liturujia inavyoadhimishwa kwa kuzingatia mambo yake ya nje. Shirikishaneni mawazo kuhusu baadhi ya mambo yafuatayo:
- Kipindi cha kiliturujia
- Rangi za kiliturujia
- Ubani
- Muundo wa sehemu takatifu ya kanisa
- Sanaa takatifu
- Muziki mtakatifu (Jambo hili linastahili kujadiliwa. Je, kuna aina bora zaidi ya muziki wa kiliturujia?)
- Ishara za mwili
- Homilia
- Sehemu ya mwisho ya Sura ya Kwanza inazungumzia umuhimu wa Umoja na Utofauti. Je, kuna yeyote mwenye maoni au ufahamu wa kushirikisha kuhusu sehemu hiyo?
Dakika 20 – Tafakari za Mwisho na kushirikishana
Mpe kila mtu nafasi kwa zamu ya kushirikisha jambo ambalo huenda limemgusa zaidi katika majadiliano au lililomchanganya zaidi, ili apate ufafanuzi au ufahamu zaidi kutoka kwa wengine.
Dakika 5 – Sala ya Kuhitimisha
Kiongozi anaanza kwa Ishara ya Msalaba na kuwaalika wote kukaa kimya kwa dakika moja, wakiwa wamefumba macho. Kila mtu atafakari yale yaliyojadiliwa, hasa jambo lililomgusa zaidi.
Kisha kiongozi anasali sala ifuatayo:
Bwana Yesu, lengo letu maishani lazima liwe kukuabudu Wewe. Tunakupenda kuliko yote tunapokuabudu kwa moyo wetu wote, akili yetu yote, roho yetu yote na nguvu zetu zote. Msaidie kila mmoja wetu kugundua uzuri na utajiri wa ibada kwa Mungu, hasa tunapoalikwa kushiriki ibada hii katika namna mbalimbali za Liturujia Takatifu.
Bwana, tunawaombea wale waliokabidhiwa majukumu maalumu katika Liturujia. Tunawaombea mapadre wetu. Waongoze, uwe pamoja nao, na uwafanye watakatifu. Daima watende kama vyombo vitakatifu na vyenyekevu vya upendo na huruma Yako.
Tunawaombea wale wanaotuongoza katika sala, usomaji wa Maandiko Matakatifu, muziki na majukumu yote ya kiliturujia. Nao pia wawe wanyenyekevu kweli, wakikuruhusu Wewe pekee kung’aa kupitia huduma yao.
Bwana, utusaidie sote kukutana Nawe kila mara tunaposhiriki Misa Takatifu, sakramenti yoyote na namna nyingine yoyote ya ibada kwa Mungu. Tukutane Nawe binafsi na kwa undani ili maisha yetu yabadilishwe.
Yesu, tunakutumainia.
Kisha kiongozi anawaalika wote waliopo kutoa sala zao wenyewe kwa namna ifuatayo (Angalizo: Hili linaweza kufanywa kwa sauti, lakini huenda ikafaa zaidi lifanywe kimya kimya, kadiri kiongozi atakavyoona inafaa):
Sasa kila mmoja wetu alete mahangaiko yake binafsi mbele ya Bwana wetu, akitumaini kwamba Yeye anatusikia na anajua yote tunayohitaji. Tumkabidhi sala hizi tukiwa na tumaini kamili kwamba anatamani kushika usukani.
(Kaeni kimya kwa dakika moja ili kila mtu azungumze na Mungu kuhusu mahitaji yake binafsi).
Kisha kiongozi anawaalika wote kuhitimisha kwa kusali Baba Yetu, Salamu Maria na Atukuzwe Baba.
Yaliyomo katika Vipindi vya Mafunzo
