Watu wengi walitandaza mavazi yao barabarani, na wengine wakatandaza matawi yenye majani waliyokuwa wamekata mashambani. Waliomtangulia pamoja na wale waliomfuata waliendelea kupaza sauti: “Hosana! Amebarikiwa anayekuja kwa jina la Bwana! Umebarikiwa ufalme ujao wa baba yetu Daudi! Hosana juu mbinguni!” (Marko 11:8–10).
Hili ndilo itikio la furaha tutakalopaza kwa Bwana wetu tunapomruhusu aingie katika roho zetu. “Hosana juu mbinguni!” Neno ‘hosana’ si mlio wa sifa bali ni ombi la wokovu. Linatokana na neno la Kiebrania lenye maana ya “okoa, tafadhali,” au “okoa sasa.” Maneno yake ya msingi yanapatikana katika Zaburi 118:25: “Utuokoe, tunakusihi, Ee Bwana!” Lazima tutoe sala hii kwa unyofu tunapoingia katika Juma Kuu, kwa sababu inagusa kiini cha ujumbe mkuu wa juma hili wenye mambo mawili: Tunahitaji Mwokozi, na Yesu ndiye Mwokozi huyo.
Je, unatambua kwamba unahitaji Mwokozi? Kwa juu juu inaweza kuwa rahisi kujibu, “Ndiyo!” Lakini utambuzi huo una kina gani ndani ya roho yako? Wakati mwingine tunaweza kuangukia katika kishawishi cha hila cha kuwaza, “Mimi ni mtu mwema; ninastahili Mbingu.” Lakini kuwaza namna hii ni kinyume na sala ya “Hosana!”
Tunapopanua sala hiyo na kusema “Hosana juu mbinguni!” tunasema, “Ee Bwana, Wewe uliye Mungu kutoka Mbinguni, utuokoe katika dhambi zetu!” Ili tusali sala hii kwa kina, kwa unyofu, na kwa namna inayokusudiwa kusaliwa, ni muhimu tutambue kwa undani jinsi tunavyomhitaji Masihi. Bila Umwilisho Wake, kifo Chake na Ufufuko Wake, tusingeokolewa. Badala yake, tungekufa katika dhambi zetu na kuishi katika taabu milele. Ukweli huo unaweza kuwa mgumu kuukubali, lakini tukiuelewa ukweli huu wa fumbo, tutaweza kupaza sauti, “Hosana juu mbinguni!”
Kutambua kwamba tunahitaji Mwokozi kunatufanya tujinyenyekeze. Lazima tukiri udhaifu wetu na kutoweza kabisa kujiokoa wenyewe. Lakini habari njema ni kwamba hatuhitaji kujiokoa wenyewe. Ingawa tumeitwa kuishi maisha ya mapendo na matendo mema, matendo hayo si chanzo cha wokovu wetu—Yesu ndiye chanzo chake. Tunapokuwa katika hali ya neema, tunapata fadhila isiyopimika ya kushiriki katika tendo Lake la upendo kwa kushiriki katika mapendo na huruma zinazotiririka katika maisha yetu kutoka katika maisha Yake, na kuwagawia wengine mapendo na huruma hizo.
Kuingia kwa Yesu kwa shangwe katika mji mtakatifu wa Yerusalemu kunaashiria kuingia Kwake katika roho yako kwa neema. Anapokujia, tandaza mbele Yake matawi ya mitende ya shukrani na heshima yako. Paza sauti, “Uniokoe, Bwana, nakusihi! Hosana juu mbinguni!” Ukiweza kujinyenyekeza leo, Jumapili ya Matawi, na kumkaribisha Mwokozi wako kwa ukamilifu zaidi ndani ya roho yako, basi mafumbo tunayoshiriki katika Juma hili Kuu yatazaa matunda mengi zaidi. Siku zinazotangulia Siku Tatu Kuu zitakuchochea kutafakari yale yanayokaribia kutokea. Alhamisi Kuu itakualika kushiriki kwa ukamilifu zaidi katika Karamu ya Ekaristi ya Mwili na Damu, Roho na Umungu wa Kristo, na itakuongoza katika maisha ya kina zaidi ya huduma ya unyenyekevu kwa kumwiga Bwana wetu. Ijumaa Kuu ndiyo siku yenye nguvu na yenye kuleta mabadiliko makubwa zaidi katika mwaka, ambapo tunashiriki katika Sadaka ya wokovu ya Msalaba wa Kristo. Hatusherehekei Misa Takatifu siku hiyo kwa sababu siku yenyewe ni chombo cha neema ya Msalaba. Jumamosi Kuu ni siku ya kungoja kwa matumaini, na Jumapili ya Pasaka ndiyo kilele cha furaha kwa ushindi wa Kristo.
Tafakari juma linalokuja na uazimie kuliishi siku moja baada ya nyingine. Anza leo kwa kujinyenyekeza na kukiri kwamba unahitaji Mwokozi, Mwokozi mmoja tu wa ulimwengu. Mpazie sauti na umsihi akuokoe.
Hosana Kwako, Bwana na Mwokozi wangu, hosana juu mbinguni! Tafadhali njoo kwangu na uniokoe. Nisaidie kuona jinsi ninavyohitaji kabisa utendaji Wako wa wokovu katika maisha yangu na kukukaribisha kwa ukamilifu zaidi katika hekalu la roho yangu. Hosana juu mbinguni! Yesu, nakutumainia.
Mengine kwa ajili ya Kwaresima
